• HABARI MPYA

    Sunday, November 26, 2017

    SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE NA LIPULI, 1-1 UHURU

    Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC wameshindwa kuutumia vizuri nafasi ya kucheza nyumbani, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Lipuli ya Iringa katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Sare hiyo inamaanisha Simba SC inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 23 baada ya mechi 11, ikiwazidi kwa pointi mbili tu mabingwa watetezi, Yanga ambao nao jana walilazimishwa sare ya 1-1 na Tanzania Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, aliyesaidiwa na Khalfan Sika wa Pwani na Vincent Mlabu wa Morogoro iliwachukua dakika 15 tu Simba kupata bao la kuongoza, lililofungwa na kiungo wake mkongwe, Mwinyi Kazimoto Mwitula.
    Beki wa Lipuli, Mghana, Asante Kwasi akimiliki mpira dhidi ya mshambuliaji wa Simba, John Bocco
    Winga wa Simba, Shiza Kichuya akimtoka beki wa Lipuli leo 
    Mshambuliaji wa Lipuli, Ramadhani Mandebe (kulia) akiwania mpira dhidi ya kiungo wa Simba, Jonas Mkude
    Kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto akipasua katikati ya wachezaji wa Lipuli leo

    Kazimoto alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi ya kiungo mwenzake, Muzamil Yassin mbele ya mstari wa kuugawa Uwanja na kutembea nayo hatua mbili kabla ya kumtungua kwa mpira wa juu kipa wa Lipuli, Agathony Mkwando aliyetokea kujaribu kuokoa. 
    Simba ilipata bao hilo ikitoka kupoteza nafasi tatu nzuri za kufunga mabao kupitia kwa nyota wake John Bocco, Shiza Kichuya na Muzamil Yassin.
    Lipuli walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika nne baadaye kupitia kwa Nahodha wao, Mghana Asante Kwasi aliyefunga kwa shuti la mpira wa adhabu.
    Baada ya baio hilo, timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu, lakini ni ndiyo waliotengenewza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia.
    Kipindi cha pili, Simba SC waliendelea kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Lipuli, lakini wakashindwa kutumia vyema nafasi nyingi walizotengeneza.
    Safu ya ulinzi ya Lipuli ikiongozwa na mabeki wa zamani wa Simba SC, Novaty Lufunga na Mganda Joseph Owino ilijitahidi kutibua mipango mingi ya safu ya ushambuliaji ya Wekundu wa Msimbazi.  
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohamed Hussen ‘Tshabalala’, James Kotei/ Ally Shomari dk71, Yusuph Mlipili, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin, John Bocco, Mwinyi Kazimoto/ Nichalaus Gyan dk65 na Haruna Niyonzima/ Laudit Mavugo dk54.
    Lipuli FC; Agathony Mkwando, Asante Kwasi, Hussein Rashid/Martin Kazila dk46, Ally Mtoni, Joseph Owino, Hamad Manzi/Novaty Lufunga dk35, Seif Karihe/ Waziri Ramadhani dk77, Mussa Nampaka, Ramadhani Mandebe, Malimi Busungu na Shaaban Ada. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE NA LIPULI, 1-1 UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top