• HABARI MPYA

  Ijumaa, Novemba 24, 2017

  KIUNGO MCAMEROON AKUBALI KUONGEZA MKATABA WA MWAKA AZAM FC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Azam FC imefikia makubaliano ya kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja kiungo mkabaji raia wa Cameroon, Stephan Kingue.
  Kiungo huyo aliyejiunga na Azam FC Novemba mwaka jana anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa ukabaji pamoja na kupiga pasi zinazofika.
  Akithibitisha nyongeza hiyo ya mkataba mbele ya waandishi wa habari leo mchana, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, alisema kuwa wamefikia uamuzi huo kufuatia mapendekezo ya Kocha Mkuu Aristica Cioaba, ambaye anataka kuendelea na huduma yake.
  “Uongozi wa juu wa Azam FC ulikuwa na mazungumzo na mchezaji Stephan Kingue Mpondo, amekuwa na timu kwa kipindi cha mwaka mmoja hivi sasa mkataba wake umekwisha na mazungumzo yalikuwa juzi na jana, lakini tunashukuru Mungu ni kwamba Stephan Mpondo kwa mujibu wa taarifa ya mwalimu Cioaba bado anamuhitaji kikosini.
  Stephan Kingue Mpondo (kushoto) amekubali kuongeza mkataba wa  mwaka mmoja Azam FC

  “Hivyo uongozi umechukua jukumu la kuongea na mchezaji huyu na ninavyoongea na nyinyi ni kuwa Mpondo atendelea kuwepo ndani ya Azam FC baada ya jana kukubaliana na uongozi na amepewa mkataba wa mwaka mmoja zaidi kwa maana ya kuendelea ndani ya timu yetu, ni mchezaji ambaye mwalimu amemkubali kwa maana ni mchezaji kiongozi uwanjani lakini moja ya sifa yake Mpondo ni nidhamu na kujituma zaidi uwanjani,” alisema.
  Wakati huo huo: Mtendaji Mkuu Msaidizi wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Humphrey Mandu ametembelea makao makuu ya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Mandu, ambaye pia ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Ligi Kuu Uganda inayodhaminiwa na Kampuni ya Azam Media kupitia Azam TV (Azam Uganda Premier League, amekuja nchini kwa ziara maalumu ya kuwatembelea wadhamini wa ligi yao Azam TV na kampuni za Azam kwa ujumla.
  Meneja wa Uwanja wa Azam FC, Sikitu Salim, ndiye aliyepokea ugeni huo na kuwatembeza maeneo mbalimbali wageni hao ndani ya Azam Complex, kama vile uwanja, gym, Media Center na vyumba wanavyolala wachezaji.
  Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mandu alisifia uwekezaji uliofanywa ndani ya Azam FC akidai kuwa ni wa kushangaza sana na kiwango cha hali juu.
  “Azam Complex ni moja ya kituo ambacho ni bora, tunafuraha na Azam kwa inachokifanya Uganda ni kitu cha kushangaza ikidhamini ligi (Azam Uganda Premier League) wakiwa wadhamini wakuu wa ligi, hivi sasa tulivyotembelea Azam Complex hapa Dar es Salaam imetupa matumaini mazuri kuwa Azam ni taasisi inayothamini soka na inaweza kuendeleza.
  “Hiyo inamaanisha kuwa tunafanya kazi na taasisi sahihi katika kusaidia maendeleo ya soka Uganda, tukiwa kama watu wa mpira tunafuraha kuona kuwa Azam imewekeza ipasavyo kwenye soka la Uganda na Tanzania, tumeona uwanja mkubwa mzuri na wa ajabu, nimewahi kufanya ukaguzi wa viwanja hapa Afrika lakini huu uwanja (Azam Complex) ni moja ya viwanja bora,” alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KIUNGO MCAMEROON AKUBALI KUONGEZA MKATABA WA MWAKA AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top