• HABARI MPYA

  Thursday, November 23, 2017

  TANZANIA YAZIDI KUPOROMOKA FIFA, SASA YA 142 DUNIANI

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  PAMOJA na sare ya 1-1 katika mchezo wa ugenini dhidi ya Benin mwezi huu, Tanzania imeporomoka kwa nafasi sita kwenye viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
  Taarifa ya FIFA inaonyesha Tanzania sasa inashika nafasi  ya 142, wakati Uganda imeendelea kuongoza kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa inashika nafasi ya 15, wakati Senegal sasa inaongoza kwa Afrika nzima. 
  10 Bora mwezi huu ni Ujerumani, Brazil, Ureno, Argentina, Ubelgiji, Hispania, Poland, Uswisi, Ufaransa na Chile.
  Sare ya 1-1 na wenyeji, Benin Novemba 12, mwaka huu katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa l'Amitie, au Urafiki mjini Cotonou ilitarajiwa kuipandisha Tanzania.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa nchini humo, Ligali Praphiou aliyesaidiwa na Bello Razack na Koutou Narcisse, hadi mapumziko wenyeji The Squirrels, walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa dakika ya 33 kwa penalti na mkongwe mwenye umri wa miaka 33, Nahodha, Stephane Sessegnon anayechezea klabu ya Montpellier ya Ufaransa.
  Hata hivyo, ilikuwa ni penalti ya mashaka, kwani mchezaji aliyeugusa mpira huo kwa mkono alikuwa ni wa Benin, Khaled Adenon lakini refa akadhani ni mchezaji wa Tanzania.
  Sessegnon akamtungua kipa namba moja wa Tanzania, Aishi Manula kufunga bao lake la 21 timu ya taifa katika mechi ya 68.
  Wachezaji wa Tanzania wakamlalamikia refa kwa kutowapa penalti dakika ya 32 kufuatia, winga Simon Msuva kuangushwa kwenye boksi baada ya kusukumwa.
  Kipindi cha pili, Tanzania ilikianza kwa nguvu na kasi zaidi wakishambulia kutokea pembeni na hatimaye kufanikiwa kupata bao la kusawazisha.
  Alikuwa ni mshambuliaji wa zamani wa Simba ya Tanzania na Dhofar SC ya Oman, Elias Maguri aliyefunga bao hilo akimalizia krosi ya winga Shiza Kichuya kutoka upande wa kushoto dakika ya 50.
  Kiungo wa Tanzania, Mudathir Yahya akatoka anachechemea baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Nurdin Issa Chona dk92. 
  Matokeo haya yanamaanisha Benin imeshindwa kulipa kwa Tanzania, kwani mara ya mwisho, zilipokutana Oktoba 12, mwaka 2014 Taifa Stars ilishinda 4-1, mabao ya Nahodha wa wakati huo, beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dakika ya 16, kiungo Amri Kiemba dakika ya 39, Thomas Ulimwengu dakika ya 49 na Juma Luizio, wakati la Benin lilifungwa na Suanon Fadel dakika ya 90.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TANZANIA YAZIDI KUPOROMOKA FIFA, SASA YA 142 DUNIANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top