• HABARI MPYA

  Saturday, November 25, 2017

  YANGA YALAZIMISHWA SARE NA PRISONS PUNGUFU CHAMAZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  LICHA ya kucheza pungufu ya mchezaji mmoja, Tanzania Prisons imefanikiwa kupata sare ya ugenini ya kufungana 1-1 na wenyeji, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Sare hiyo inaifanya Yanga SC iendelee kukamata nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Simba na Azam ambazo pia zina mechi moja moja mkononi. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na Shomary Lawi wa Kigoma aliyesaidiwa na Abdallah Rashid wa Pwani na Sylvester Mwanga wa Kilimanjaro, hadi mapumziko tayari timu hizo zilikuwa zimekwishafungana mabao hayo.
  Kiungo wa Yanga, Raphael Daudi akimdhibiti mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Eliuter Mpepo leo Chamazi 
  Mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa akijivuta kupiga shuti 
  Beki wa Prisons, Michael Ismail akiteleza kuondosha mpira miguuni mwa beki wa Yanga, Gardiel Michel

  Prisons walitangulia kwa  bao la Eliuter Mpepo dakika ya tisa akitumia makosa ya mabeki wa kati wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ waliochanganyana na kipa wao, Mcameroon, Youth Rostande na kushindwa kuokoa.
  Prisons walipata pigo dakika ya 36 baada ya mchezaji wake, Lambert Sibiyanka kutolewa kwa kadinyekundu na refa Lawi kufuatia kumpiga kiwiko beki wa Yanga, Juma Abdul.
  Yanga walitumia mwanya huo kuongeza mashambulizi kusaka bao la kusawazisha na wakafanikiwa kupata bao dakika ya 41, lililofungwa na kiungo Raphael Daudi aliyemalizia krosi ya mshambuliaji Ibrahim Ajib.
  Kipindi cha pili, Yanga walikianza kwa kasi wakishambulia kwa mipira ya kutokea pembeni hadi wakafanikiwa kupata bao lingine, lililofungwa na mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyemalizia krosi ya beki Gardiel Michael kutoka kushoto – lakini refa Lawi akalikataa akisema mfungaji a,likuwa ameotea.  
  Prisons waliokuwa wakicheza vizuri katika eneo la katikati ya Uwanja, walifanikiwa kuwazuia Yanga kupata mabao zaidi, licha ya mabingwa hao watetezi kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa timu ya jeshi la Magereza nchini. 
  Kwa sare hiyo, Yanga inafikisha pointi 21 baada ya kucheza mechi 11, ikizidiwa pointi mbili mbili na zote, Simba na Azam. Simba watawakaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Uhuru kesho na Azam watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Chamazi Jumatatu.   
  Kikosi cha Yanga SC; Youthe Rostand, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Kelvin Yondan dk46, Pato Ngonyani, Pius Buswita, Raphael Daudi, Obrey Chirwa, Ibrahim Ajib/Yussuf Mhilu dk85 na Emmanuel Martin/Geoffrey Mwashiuya dk73.
  Tanzania Prisons; Aaron Kalambo, Michael Ismail, Laurian Mpalile, Nurdin Chona, James Mwasote, Jumanne Elfadhil, Salum Kimenya/Fredy Chudu dk58/Kazungu Mashauri dk77, Kassim Hamisi, Eliuter Mpepo/Hamisi maingo dk74, Mohammed Rashid na Lambert Sibiyanka.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YALAZIMISHWA SARE NA PRISONS PUNGUFU CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top