• HABARI MPYA

    Sunday, November 26, 2017

    IBRAHIM CLASS ATETEA TAJI LA GBC, AMSHINDA MSAUZI KWA POINTI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BONDIA Mtanzania, Ibrahim Class Mgendera usiku huu amefanikiwa kutetea taji lake GBC uzito wa Light baada ya kumshinda kwa pointi Koos Sibiya wa Afrika Kusini.
    Mgendera alishinda kwa pointi za majaji wote, ingawa ushindi wake ulilalamikiwa na mpinzani wake baada ya pambano hilo.
    Haukuwa ushindi wa mashaka, kwani Mgendera alipigana vizuri kwa tahadhari kuanzia raundi ya kwanza hadi ya 10 akipiga ngumi za kudonoa kwa wingi katika staili yake ya Orthodox.
    Refa kutoka Ujerumani akimuinua mkono Ibrahim Class kumtangaza mshindi usiku wa Jumamosi Uwanja wa Uhuru
    Ibrahim Class (kulia) akipambana na Koos Sibiya ulingoni
    Waziri wa Habari Utamadunia Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akimpongeza Ibrahim Class
    Ibrahim Class (kushoto) akimuadhibu Koos Sibiya ulingoni 

    Mgendera hakuwa na kazi nyepesi ulingoni, kwani alikutana na bondia mzoefu na mwenye ngumi nzito – lakini akahimili vishindo vyote na kuwafurahisha Watanzania wachache waliojitokeza Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kumshangilia kwa mchezo mzuri.
    Dalili za Mgendera kushinda pambano hilo zilianza kuonekana raundi ya nane baada ya kumjeruhi kwenye pua Sibiya ambaye alichafuka damu eneo hilo hadi mdomoni.
    Na ni kuanzia raundi hiyo bondia wa Tanzania alianza kutawala pambano baada ya wawili hao kuonekana kupigana sawa katika raundi zilizotangulia.  
    Mgendera aliyezaliwa Oktoba 10, mwaka 1990 eneo la Ipogolo, wilayani Mufundi mkoani Iringa, alitwaa taji hilo Julai 1, mwaka huu baada ya kumpiga Jose Luis Forero Atencio wa Panama kwa pointi Jijini Berlin, Ujerumani.  
    Hilo linakuwa pambano la 21 Mgendera kushinda kati ya 25 aliyocheza, akiwa amepoteza mapambano manne. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: IBRAHIM CLASS ATETEA TAJI LA GBC, AMSHINDA MSAUZI KWA POINTI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top