• HABARI MPYA

  Saturday, November 25, 2017

  MGOSI AMUAMBIA BOCCO; “ONGEZA MAZOEZI UWE FITI UTATISHA SANA SIMBA”

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi amemshauri mshambuliaji wa sasa wa klabu hiyo, John Raphael Bocco aongeze mazoezi ili awe fiti zaidi aweze kung’ara Msimbazi.
  Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mgosi amemuambia Bocco kwamba anaweza kuwa mchezaji muhimu iwapo tu ataongeza bidii ya mazoezi na kuwa fiti zaidi.
  “Asante kijana wangu, mimi ninajua kwa aina yako wewe ni mchezaji unayehitajika sana Simba, ongeza feetness ili wengine nao waamini hiki ninachokiamini mimi,”aliandika Mgosi.
  Na Mgosi aliyewahi pia kuchezea Mtibwa Sugar ya Morogoro, JKT Ruvu ya Dar es Salaam na Daring Club Motema Pembe (DCMP) ya Kinshasa aliposti ujumbe huo ulioambatana na picha ya Bocco baada ya mchezaji huyo kuifungia Simba bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons Jumamosi iliyopita Mbeya.
  Mussa Hassan Mgosi amemshauri John Bocco aongeze mazoezi ili awe fiti zaidi aweze kung’ara MsimbazI
  Bocco alifunga bao zuri dakika za mwishoni baada ya kumiliki mpira vizuri akiwa amezingirwa na mabeki wa Prisons na kugeuka nao kabla ya kufumua shuti kali lililotinga nyavuni na kuifanya Simba iendelee kuongoza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Ushindi huo, uliifanya Simba ifikishe pointi 22 baada ya kucheza mechi 11, wakifuatiwa na Azam FC wenye pointi 22 pia, wakati Yanga wapo nafasi ya tatu kwa pointi zao 20. Simba watashuka tena dimbani kesho kumenyana na Lipuli ya Iringa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Ligi Kuu iliendelea jana kwa mchezo mmoja tu, wenyeji Ndanda FC wakilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Njombe Mji FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
  Mechi nyingine za leo, Singida United watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Namfua, Singida, Mbao FC wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Kagera Sugar wataikaribisha Stand United Uwanja wa kambarage Shinyanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Maji Maji Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. 
  Na mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu inayoonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV utakamilishwa Jumatatu ijayo kwa mchezo mmoja kati ya wenyeji, Azam FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MGOSI AMUAMBIA BOCCO; “ONGEZA MAZOEZI UWE FITI UTATISHA SANA SIMBA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top