• HABARI MPYA

  Sunday, October 08, 2017

  YANGA YATOKA SARE NA KMC 0-0 CHAMAZI

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga Sc, wameshindwa kutamba mbele ya timu ya Manispaa ya Kinondoni KMC, na kutoka sare ya 0-0, katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi.
  Katika mechi hiyo Yanga wameonekana bado wanaandamwa na tatizo katika eneo la ushambuliaji kutokana na kutengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia.
  Kiungo wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi akimtoka mchezaji wa KMC jana 
  Beki anayewania kusajiliwa Yanga, Mkongo Festo Kayembe akimtoka mchezaji wa KMC
  Kiungo wa Yanga, Maka Edward akimpita mchezaji wa KMC

  Katika kipindi cha kwanza kwenye mchezo huo, Yanga walitengeneza nafasi nyingi ambapo katika dakika ya nne ya mchezo huo Yusuph Mhilu alijaribu kutaka kuifungia Yanga bao la kuongoza kwa shuti kali lakini anapiga ubavuni mwa nyavu.
  Dakika ya 11 Emanuel Martin alijaribu pia kuttaka kufunga bao kwa shuti la mbali lakini shuti lake linakwenda nje.
  Yanga waliendelea Kuliandama lango la KMC kwa mashambulizi ya mara kwa mara, ambapo dakika ya 20 Mhilu tena alishindwa kuipatia timu yake bao kwa kushindwa kumalizia krosi nzuri iliyoingizwa na Mwashiuya na shuti lake dhaifu lilikwenda nje.
  Dakika ya 27, Maka Edward anaingiza krosi nzuri inayokwenda moja kwa moja langoni mwa KMC lakini umakini wa kipa wa timu hiyo, Yusuph Abdul aliokoa hatari hiyo.
  Kipa huyo wa KMC ndiyo unaweza kusema alikuwa ni nyota wa mchezo huo kutokana na kufanya kazi kubwa na kuondosha hatari nyingi langoni kwake.
  KMC walionekana kuwa vizuri sana na kama isingekuwa uzoefu wa Yanga, timu hiyo wangeweza kutoka na matokeo mazuri na dakika ya 30 Michael Chindu nusura aipatie timu hiyo bao kwa pasi ya Godfrey Sabas lakini kipa wa Yanga Beno Kakolanya anaokoa hatari
  [Andrwe Vincent Dante alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 32 kwa kumchezea rafu Ally Ramadhan.
  Dakika ya 36 Matheo Antony anaambaa ambaa na mpira kutoka katikati ya uwanja na kupiga shuti kali nje ya 18 lakini kipa wa KMC alifanya kazi kubwa kupangua hatari hiyo langoni kwake.
  Hassan Ramadhan Kessy alionyeshwa kadi ua njano dakika ya 44 na mwamuzi wa mchezo huo, Said Pambaleo baada ya kupingana na maamuzi ya mwamuzi huyo.
  Hadi zinakwenda mapumziko timu hizo hakuna aliyefanikiwa kutikisa nyavu za mpinzani wake.
  Kipindi cha pili kilianza kwa Kasi Yanga wakionyesha kulitafuta bao kwa nguvu.
  Dakika ya 46 KMC walifanya mabadiliko alitoka Michael Chindu na nafasi yake alichukua Kagare Mgunda.
  Yanga pia walifanya mabadiliko dakika ya 57 alitoka  Kessy akaingia Juma Abdul na alitoka Yusuph Mhilu nafadi yake akachukua Burhan Akilimali.
  Dakika 71 Mwinyi Ally nusura aipatie KMC bao kwa shuti la faulo nje ya 18 lakini kipa wa Yanga aliucheza mpira. Dakika ya 76 KMC alitoka Erick Mawala akaingia Fredson Kazambuga.Dakika ya 86 KMC tena alitoka  Ally Ahmed akaingia namba 32.
  Yanga walionekana kubadilika sana kwenye dakika za mwishoni na kushambulia zaidi baada ya kuingia Juma Abdul na Akilimali lakini walishindwa kupata bao.
  Hadi dakika ya 90 ya mchezo huo inamalizika timu hizo zlitoka zikiwa zimetoshana nguvu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YATOKA SARE NA KMC 0-0 CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top