• HABARI MPYA

  Sunday, October 08, 2017

  KAMA MFUMO WA KOCHA MAYANGA HAUTAKI WASHAMBULIAJI, TULIE NA NANI?

  SEPTEMBA 23, mwaka huu wakati kocha Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Shaaban Mayanga anataja kikosi cha kucheza na Malawi aliwafurahisha wengi kwa kumrejesha mshambuliaji Ibrahim Hajib wa Yanga.
  Lakini hakuwaita wachezaji wawili wanaocheza nje, kiungo Farid Mussa wa Tenerife ya Hispania na Elias Maguri wa Dhofar FC ya Oman.
  Mchezo uliotangulia dhidi ya Botswana Taifa Stars ikishinda 2-0 Septemba 2, mwaka wote waliitwa na wakatokea benchi, Maguli akiingia dakika ya 82 kumpokea Nahodha Mbwana Samatta na Farid Mussa dakika ya 66 kuchukua nafasi ya Shiza Kichuya.
  Haikuwa ajabu Maguli na Mussa wote kutoitwa safari hii, kwa kuwa hawakidhi mahitaji ya kocha Mayanga kwa sababu tofauti.
  Kiwango cha Mussa kimeshuka tangu ahamie Hispania kutoka Azam FC mwaka jana na Maguli anaangushwa na mfumo anaotumia kocha Mayanga, ambao hauhitaji mshambuliaji zaidi ya mmoja na kwa sababu hiyo inabidi washambuliaji wote nchini wapange foleni nyuma ya Samatta.
  Mshambuliaji chipukizi na mfungaji mzuri anayeinukia, Mbaraka Yussuf jana ameingizwa dakika ya 54 kwenda kuchukua nafasi ya kiungo ya Raphael Daudi.
  Mayanga jana alianzisha mshambuliaji mmoja tu, Nahodha Saamtta ambaye alimaliza tofauti na Septemba 2 alimpisha Maguli ambaye jana hakuwepo kabisa.  
  Kikosi cha jana; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Abdi Banda, Kevin Yondan, Himid Mao, Simon Msuva/Abdul Hilal dk85, Hamisi Abdallah/Muzamil Yassin dk14, Mbwana Samatta, Raphael Daudi/Mbaraka Yussuf dk54 na Shiza Kichuya/Ibrahim Hajib dk58.
  Kikosi cha Septemba 2 dhidi ya Botswana; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Abdi Banda, Kevin Yondan, Himid Mao, Simon Msuva/Emmanuel Martin dk82, Hamisi Abdallah/Said Ndemla dk80, Muzamil Yassin/Raphael Daudi dk57, Mbwana Samatta/Elias Maguli dk82 na Shiza Kichuya/Farid Mussa dk66.
  Baada ya kutomuita kwa muda mrefu tangu achukue nafasi ya Charles Boniface Mkwasa Machi mwaka huu, Mayanga alimuita kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha COSAFA, michuano iliyofanyika nchini Afrika Kusini Julai.
  Na hakuna shaka mchezaji huyo wa Dhofar SC ya Oman alifanya vizuri kwenye COSAFA akifunga bao pekee kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya wenyeji, Afrika Kusini na wengi waliamini baada ya mechi za kufuzu CHAN dhidi ya Rwanda angeitwa tena na kweli akaitwa kwenye mchezo dhidi ya Botswana.
  Alipewa dakika nane tu, lakini wote tuliona Maguli alikwenda kuutendea haki muda ule mfupi na alikaribia kufunga. Lakini ajabu hakuitwa kwa ajili ya mchezo uliopita ambao tumelazimishwa sare na Malawi nyumbani, 1-1 jana.
  Unapokuwa na kocha wa taifa aina ya Mayanga ni vigumu kuwainua washambuliaji chipukizi, kwa sababu tayari yeye si muumini wa mfumo wa kutumia washambuliaji na macho yake yanamulika zaidi viungo na walinzi.
  Wakati wa mechi za CHAN dhidi ya Rwanda, alimuita John Bocco na akamchezesha kama mshambuliaji pekee Mwanza na Kigali timu ikilazimishwa sare 1-1 nyumbani na 0-0 ugenini hivyo kutolewa kwa mabao ya ugenini.
  Kikosi cha Stars dhidi ya Amavubi Julai 15 Mwanza; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Nurdin Chona, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Simon Msuva, Himid Mao, John Bocco/Stahmili Mbonde dk93, Muzamil Yassin na Shiza Kichuya.
  Kikosi cha Stars dhidi ya Rwanda Julai 22 Kigali; Aishi Manula, Boniphace Maganga, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Salim Mbonde, Himid Mao, Simon Msuva/Joseph Mahundi dk66, Muzamil Yassin, John Bocco ‘Adebayor’, Raphael Daudi/Said Ndemla dk62 na Shiza Kichuya.
  Katika mchezo wa jana, Mayanga hakuwaita Bocco na Mbonde japokuwa wote wapo fiti na badala yake akawaita Samatta kama kawaida, Hajib ambaye hakuna uhakika kama kambi ijayo atarejeshwa na Mbaraka.
  Tu kwa sababu yeye hataki washambuliaji – na ataendelea kumulika mawinga na viungo kutoka popote, lakini kwake mshambuliaji Samatta anatosha.
  Tunapaswa kuheshimu maamuzi ya kocha wetu wa taifa na hususan tukizingatia rekodi yake si mbaya hadi sasa, lakini pia tunapaswa kukumbuka kwamba kama tunahitaji ushindi na mabao lazima tuwe na washambuliaji.
  Bahati nzuri tunao washambuliaji na wafungaji wazuri akina Mbaraka, Maguli, Mbonde, Bocco na Samatta – lakini mbele ya mfumo wa kocha wa Taifa Stars wa sasa hawana thamani.
  Washambuliaji wetu wametudhihirishia uwezo wao kwa kufunga kwenye mechi za timu ya taifa, lakini wanakatishwa tamaa na mfumo wa kocha Mayanga ambao hauwahitaji.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAMA MFUMO WA KOCHA MAYANGA HAUTAKI WASHAMBULIAJI, TULIE NA NANI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top