• HABARI MPYA

  Wednesday, October 11, 2017

  YANGA KUMENYANA NA RHINO RANGERS OKTOBA 18 TABORA

  Na Adam Hhando, TABORA 
  KLABU ya Rhino Rangers ya Tabora inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,Yanga SC Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora Oktoba 18, mwaka huu.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ukumbi wa Muungano Mesi mjini hapa, Katibu Mkuu wa Rhino, Dickson Mgalike amesema kwamba Yanga itawasili mkoani Tabora Jumatatu ya Oktoba16 ikitokea Kagera, ambako Jumamosi wiki hii itacheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba.
  “Yanga ikimaliza mchezo wao dhidi ya Kagera itaanza safari ya kuja Tabora na siku ya Jumatatu (Oktoba 16/) itawasili hapa tayari kwa ajili ya mchezo huo, na mipango yote inaendelea kuelekea mchezo huo,”alisema Mgalike.
  Kiungo wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi ataonekana Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora Oktoba 18, mwaka huu  
  Amesema makocha wa timu hiyo, Amatre Richard na Danny Mwang’ombe watautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya michezo ijayo ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Pamba FC na Toto Africans mechi, ambazo zitapigwa Oktoba 22 na 28 Jijini Mwanza.
  Kwa Yanga, watautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya mpambano wa raundi ya saba ya Ligi Kuu dhidi ya Stand United ya Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga Oktoba 22, mwaka huu.
  Rhino inashika nafasi ya sita katika kundi C, nyuma ya vinara wa kundi hilo Alliance ya Mwanza kwa pointi zao 10, wakifuatiwa na Dodoma FC ya Dodoma yenye pointi tisa, wakati JKT Oljoro ina pointi sita, Toto Africans na Transit Camp kila moja pointi nne.
  Mara ya mwisho Yanga kucheza Tabora ilikuwa Oktoba 31, mwaka 2015 walipokuja kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar ambayo wakati huo ilikuwa inautumia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
  Ikiwa imepita siku 17 tu kwa mashabiki wa soka mkoani Tabora tangu wawashuhudie vigogo wengine wa soka nchini, Simba SC wakicheza mchezo wa kirafiki na Milmabo FC ya hapa, fursa nyingine ya burudani ya soka inawadia wiki ijayo kwa Yanga kuja kucheza Rangers.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KUMENYANA NA RHINO RANGERS OKTOBA 18 TABORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top