• HABARI MPYA

  Saturday, October 07, 2017

  TFF YAOMBOLEZA MSIBA WA REFA WA MAJI MAJI NA YANGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya wanafamilia wawili wa soka vilivyotokea Oktoba 5, 2017 kwa nyakati tofauti.
  Taarifa ambazo TFF imezipata zinasema waliofariki dunia siku hiyo ni aliyekuwa Mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’; Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’; pamoja na Afrika Mashariki miaka ya 1950 na 1960, Abdul Majham na Mwamuzi wa Daraja la Kwanza anayechezesha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Mirambo Tshikungu.
  “Hakika nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo hivi. Ni mshtuko mkubwa sana katika familia ya mpira wa miguu hapa Tanzania, natambua pia ni majonzi makubwa kwa familia za marehemu,” amesema Rais Karia.
  “Niombe tu kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, majirani kuwa watulivu katika kipindi hiki cha msiba. Wawe na moyo wa subira baada ya ndugu zetu kutanguliwa mbele ya haki.
  Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwingi wa Rehema, basi na tumuombe awe na msamaha kwa ndugu zetu,” amesema.
  Abdul Majham aliyefariki dunia huko Visiwani Zanzibar ni Mchezaji huyo wa zamani wa Klabu ya Vikokotoni ya  visiwani Zanzibar, pia aliyepata kuichezea klabu Bingwa ya kwanza ya Tanzania, Cosmopolitan ya Dar es Salaam.
  Kuhusu Tshikungu, TFF imepokea taarifa inayosema kwamba alifariki dunia jioni ya Oktoba, 2017 katika Hospitali ya Ikonda iliyoko Wilaya ya Makete mkoani Njombe alikokuwa akitibiwa.
  Mwenendo wa uchezeshaji wake ulikuwa na tija kwani rekodi zinaonesha kwamba mchezo wake mkubwa kuuchezesha msimu uliopita ulikuwa ni kati ya Majimaji ya Songea na Yanga SC ya Dar es Salaam uliofanyika Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF YAOMBOLEZA MSIBA WA REFA WA MAJI MAJI NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top