• HABARI MPYA

  Monday, October 09, 2017

  SALAH AIRUDISHA MISRI KOMBE LA DUNIA BAADA YA MIAKA 28

  NYOTA wa Liverpool, Mohamed Salah usiku wa jana alikuwa shujaa baada ya kufunga kwa penalti dakika ya 95 na kuiwezesha Misri kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 28, kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya Kongo katika mchezo wa Kundi E.
  Mchezo ukiwa kwenye dakika za majeruhi, Salah akaenda kupiga penalti ngumu ambayo timu yake ilizawadiwa na kuwainua kwa furaha kubwa mashabiki waliofurika Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.
  Nyota wa Liverpoo, Mohamed Salah akiwa amebebwa baada ya kuifungia mabao yote mawili Misri ikirejea Kombe la Dunia jana PICHA ZAIDI GONGA HAPA 

  Kuanzia hapo, sherehe zilkuwa kubwa Misri nzima mashabiki wakiwa na jenzi zao nyekundu na wananchi wakiingia mitaani kushangilia, magari yakiranda huku yanapiga ving'ora na honi, furaha za Mafarao kurejea Kombe la Dunia. 
  Mjini Cairo, helikopta ya jeshi ilimwaga maelfu ya bendera ya Misri katika eneo maarufu kama Tahrir.
  Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi amewapongeza watu Misri baada ya mechi hiyo huku mashabiki wasiochoka wakimiminika mitaani na bendera zao na jezi nyekundu na nyeusi kushangilia mafanikio hayo. 
  Kongo walikaribia kuvuruga sherehe za wenyeji, wakati Arnold Bouka kuisawazishia bao timu yake dakika ya 87, kufuatia Salah kufunga la kwanza dakika ya 63. 
  Matokeo haya yanamaanisha Mafarao wa Misri watarejea Kombe Ia Dunia nchini Urusi mwakani kwa mara ya kwanza tangu waliposhiriki fainali za mwaka 1990.
  Kikosi cha Hector Cuper kiliingia kwenye mchezo wa jana kikijua ushindi utawahakikishia nafasi ya kwenda Urusi hata kabla ya kucheza mechi yao ya mwisho, baada ya juzi Uganda kutoka sare ya 0-0 na Ghana mjini Kampala.
  Misri imeshinda mataji manne ya Kombe la Mataifa ya Afrika tangu mwaka 1990 -katika miaka ya 1998, 2006, 2008 na 2010 - lakini imeshindwa kufuzu Kombe la Dunia kipindi chote hicho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SALAH AIRUDISHA MISRI KOMBE LA DUNIA BAADA YA MIAKA 28 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top