• HABARI MPYA

  Thursday, October 12, 2017

  MSUVA AIFUNGIA BAO MUHIMU DIFAA IKICHAPWA 2-1 UGENINI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva jana ameifungia timu yake, Difaa Hassan El - Jadida bao muhimu la ugenini ikifungwa 2-1 katika mchezo wa Kombe la Ligi Morocco na Chabab Rif Hoceima Uwanja wa Mimoun Al Arsi mjini Al Hoceima.
  Kwa bao hilo, Difaa Hassan El – Jadida watahitaji ushindi wa 1-0 tu nyumbani kwenye mchezo wa marudiano wiki ijayo ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo. 
  “Nina furaha nimefunga bao, japokuwa tumefungwa 2-1 lakini kwenye mchezo wa ugenini, tunaelekeza nguvu zetu kwenye mchezo wa marudiano tuweze kushinda na kusonga mbele,”amesema Msuva akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online mapema leo.
  Simon Msuva akipongezwa na wenzake baada ya kufunga jana
  Simon Msuva akipongezwa na mchezaji mwenzake jana
  Simon Msuva mara tu baada ya kufunga jana
  Simon Msuva akipambana kwenye mchezo wa jana Uwanja wa Mimoun Al Arsi mjini Al Hoceima

  Huo ni mwendelezo wa mwanzo mzuri kwa Msuva tangu ahamie timu hiyo miezi miwili iliyopita kufuatia kucheza Tanzania kwa muda mrefu.
  Na hilo linakuwa bao lake la nane tangu amejiunga na timu hiyo la pili kwenye mechi za mashindano, mengine sita akifunga kwenye mechi za kirafiki, zikiwemo za ziara ya Hispania.  
  Msuva alisaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na DHJ Julai 28, mwaka huu baada ya kucheza  Yanga ya nyumbani, Tanzania tangu mwaka 2012 akitokea Moro United iliyokuwa tayari imehamishia maskani yake Dar es Salaam kutoka Morogoro.
  Awali ya hapo, Msuva alipitia akademi ya Azam akitokea kituo cha kukuza vipaji vya wanasoka chipukizi, Wakati Ujao baada ya kuibuliwa na iliyokuwa taasisi ya Pangollin ya kocha Charles Boniface Mkwasa, ambaye sasa ni Katibu wa Yanga, klabu aliyoichezea na kuifundisha awali.. 
  Na baada ya kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mfungaji bora mara mbili – Msuva amehamia Morocco kusaka changamoto mpya na mafanikio zaidi kisoka.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MSUVA AIFUNGIA BAO MUHIMU DIFAA IKICHAPWA 2-1 UGENINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top