• HABARI MPYA

  Thursday, October 05, 2017

  MKOPI ASEMA KWA KOCHA MPYA MRUNDI MBEYA CITY ITATISHA MSIMU HUU

  Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
  MSHAMBULIAJI wa Mbeya City, Mohammed Mkopi amesifu ufundishaji wa kocha mpya, Mrundi, Nsanzurimo Ramadhani aliyeanza kazi juzi. 
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana mjini hapa, Mkopi ambaye amekwishaichezea MCC kwa jumla ya dakika 365 hadi sasa, amesema kocha Ramadhani ni mzuri kutokana na mafundisho yake na wanatarajia makubwa kutoka kwake. 
  “Mwalimu Ramadhani tumeanza naye vizuri mazoezi hapa Shinyanga, na tumeona makali yake kwa macho yetu. Mtindo anaotumia kufundishia, namna na jinsi anavyotuonyesha kwa mifano ni ishara tosha kuwa msimu huu utakuwa moto sana kwa City,”alisema Mkopi ambaye katika mchezo uliopita dhidi ya Mwadui alifunga bao lake la kwanza akiwa na jezi ya rangi ya zambarau dakika ya 78 timu hizo zikitoka sare ya 2-2.
  Mohammed Mkopi amemsifu kocha mpya Mrundi wa Mbeya City, Nsanzurimo Ramadhani aliyeanza kazi juzi 
  Mkopi ni kati ya wachezaji 23 waliopo hapa Shinyanga na kikosi cha Mbeya City wakiwa wameweka kambi ya kujiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC wiki ijayo.
  Mbeya City watakuwa wageni wa Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Oktoba 13, mwaka huu wakitoka kufungwa 2-1 na Stand United Shinyanga mjini kabla ya kutoa sare ya 2-2 na Mwadui huko Kishapu
  Mkopi alisajiliwa msimu uliopita MCC, lakini hakuitumia timu hiyo baada ya kufungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa tuhuma za kusajili timu mbili. “Nilivumilia msimu mzima baada ya bodi ya ligi kunipatia hukumu ya kutojihusisha na soka kwa msimu mzima, wakati wote wa adhabu yangu nilikua na maumivu, lakini sikuwa na namna zaidi ya kuwa mvumilivu na kusubiri wakati ufike,”. 
  “Na nina imani huu ni wakati bora zaidi kwangu na nina matumaini baada ya kupachika wavuni goli langu la kwanza katika mchezo uliopita dhidi ya Mwadui, neema ya magoli itaanza kumiminika kwangu binafsi na kwa wachezaji wenzangu wote. Ninataraji kuwa msimu huu tutafunga magoli mengi na kuipatia pointi nyingi timu yetu,” alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MKOPI ASEMA KWA KOCHA MPYA MRUNDI MBEYA CITY ITATISHA MSIMU HUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top