• HABARI MPYA

    Sunday, October 15, 2017

    BAO LA DAKIKA YA MWISHO LA OKWI LAINUSURU SIMBA KULALA KWA MTIBWA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BAO la Emmanuel Aronld Okwi dakika ya 90 na ushie limeunusuru Simba kulala mbele ya Mtibwa Sugar ya Morogogo baada ya kupata sare ya 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Matokeo hayo, yanaifanya Simba na Mtibwa Sugar zote zifikishe pointi 12 baada ya kucheza mechi sita, sawa na Azam FC na Yanga, za Dar es Salaam pia.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Shakaile Shangalai kutoka Pwani, aliyesaidiwa na Janet Balama wa Iringa na Sylvester Mwanga wa Kilimanjaro, hadi mapumziko Mtibwa Sugar walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Emmanuel Okwi akishangilia baada ya kuifungia bao la kusawazisha Simba dakika ya mwisho. Picha ndogo ni kipa Benedictor Tinocco akiruka bila mafanikio baada ya shuti la Mganda huyo
    Emmanuel Okwi akituliza mpira kiufundi katika mchezo huo Uwanja wa Uhuru
    Kipa Aishi Manula akiokoa moja ya hatari zilizoelekezwa langoni mwake leo
    Beki Cassian Ponera akiokoa dhidi ya mshambuliaji wa Simba, John Bocco

    Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji mwenye mwili mkubwa mithili ya Romelu Lukaku wa Manchester United, Stahmili Mbonde dakika ya 35 kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona uliopagwa na beki wa zamani wa Simba, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’.
    Pamoja na kuondoka uwanjani wako nyuma kwa bao 1-0, lakini ni Simba waliocheza vizuri zaidi kipindi cha kwanza na kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Mtibwa Sugar, ingawa tu wakashindwa kutumia nafasi.
    Kipindi cha pili, kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog alikianza kwa kufanya mabadiliko katika safu yake ya ulinzi, akimtoa beki Salim Mbonde aliyeumia na kumuingiza Mganda, Juuko Murshid.
    Hata hivyo, Mtibwa Sugar wakaendelea kung’ara uwanjania na dakika ya 51 Mbonde akapoteza nafasi ya wazi ya kufunga tena baada ya pasi nzuri ya Salum Khamis, akapiga shuti dhaifu lilikodakwa na kipa Aishi Manula.
    Mtibwa Sugar ilipata pigo dakika ya 57, baada ya Mbonde kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake anaingia Kelvin Sabato Kongwe.
    Kipa Benedictor Tinocco wa Mtibwa akaokoa shuti la Okwi aliyepokea pasi nzuri ya Jonas Mkude dakika ya 61 na dakika ya 72 kiungo Hassan Dilunga naye akapiga shuti dhaifu baada ya pasi nzuri ya Kelvin Sabato likaishia mikononi mwa Manula.
    Dakika ya 90 na ushei, beki Cassian Ponera akamvuta beki wa Simba nje kidogo ya boksi na refa Shakaile Shangalai akatenga mpira wa adhabu ambao Okwi alikwenda kupiga kiufundi na kuisawazishia Simba.
    Kipa wa Mtibwa Sugar, Tinocco aliyefanya kazi nzuri leo alitoka uwanjani analia baada ya bao hilo. 
    Kikosi cha Simba kilikuwa; Aishi Manula, Ally Shomari, Erasto Nyoni, Salim Mbonde/Juuko Murshid dk46, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Said Ndemla dk63, James Kotei, John Bocco, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima.
    Mtibwa Sugar; Benedict Tinoco, Salum Kanoni, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Dickson Daud, Cassian Ponera, Shaaban Nditi, Salum Kihimbwa/Henry Joseph dk89, Mohamed Issa, Stahmil Mbonde/Kevin Sabato dk57, Salum Khamis/Hassan Dilunga dk69 na Ally Makarani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAO LA DAKIKA YA MWISHO LA OKWI LAINUSURU SIMBA KULALA KWA MTIBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top