• HABARI MPYA

    Friday, March 17, 2017

    BALOZI WA AFRIKA KUSINI AISIFU AZAM, KIGOGO WA TFF AITABIRIA USHINDI SWAZILAND

    Na Mwandishi Wetu, PRETORIA
    BALOZI wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Richard Lupembe, ameweka wazi kuwa Azam FC ni moja ya timu zinazowatia moyo kama Watanzania wanoishi nje ya nchi, huku akiipa mkono wa ushindi kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Mbabane Swallows ya Afrika Kusini.
    Lupembe alitoa kauli hiyo wakati alipoitembelea timu hiyo jana kwenye kambi yake katika Hoteli ya Acardia jijini Pretoria, nchini humo ikijiandaa na mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo nchini Swaziland Jumapili hii saa 10.30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
    “Kwa kweli nimefarijika sana kwa kuiona Azam FC tena kama nakumbuka mlikuja hapa mwaka jana, mlikuja hapa kucheza (vs Bidvest) na nikawa mgeni rasmi na mkono wangu ukawa wa kheri mkashinda, nawahakikishieni nitawashika tena mkono na ninauhakika mtashinda tena,” alisema Lupembe.
    Balozi Richard Lupembe amesema Azam FC ni moja ya timu zinazowatia moyo kama Watanzania wanoishi nje ya nchi 

    Alisema kuwa atakuwa pamoja na timu hiyo kwa kipindi chote itakapokuwa jijini hapa hadi Jumamosi itakapoelekea Swaziland huku akiitakia kila la kheri kuelekea mtanange huo unaosubiriwa na mashabiki wengi wa timu hizo.
    “Ndio tunafahamu kuwa kuna timu kubwa za Simba na Yanga, lakini Azam FC inatia moyo kwa sisi watu ambao tulioko nje nawatakia kila la kheri, mazoezi mema mimi nipo hapa kama balozi, na nitahakikisha nitakuwa na nyie mpaka siku mtakapoenda kucheza mpira,” alisema,
    Lupembe aliitembelea Azam FC jioni wakati ikielekea kwenye mazoezi kujiandaa na mchezo huo.
    Mara mwisho Balozi huyo kuishika mkono Azam FC iliichapa Bidvest Wits mabao 3-0 jijini Johannesburg katika mchezo wa raundi kama hii, ambapo kutokana na ushindi wa 1-0 katika mchezo wa kwanza kwa sasa timu hiyo inahitaji ushindi wowote au sare ili iweze kusonga mbele.
    Wakati huo huo: Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, aliyeambatana na Azam FC kuelekea mchezo wake wa marudiano dhidi ya Mbabane Swallows, amesema wana uhakika mkubwa wa timu hiyo kusonga mbele 
    Karia ameambatana na kigogo mwingine wa TFF ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo, James Muhagama, wote kwa pamoja wakiwa na imani kubwa na timu hiyo ambayo iliondoka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani.
    Karia alisema kuwa mchezo huo ni muhimu kwa Azam FC kuweza kushinda, huku akidai kuwa ina mahesabu mazuri kutokana na kuondoka na ushindi katika mchezo wa kwanza.
    “Ukiangalia kimahesabu wao ndio wanamahesabu mazuri, na ndio maana hapa kuna uwakilishi mzito umekuja kutoka TFF tupo wawili, tunauhakika ya kwamba tutafanya vizuri, Azam FC kwa sasa wapo vizuri,” alisema.
    Karia alitoa ushauri kwa wachezaji wa timu hiyo kuzingatia nidhamu ya mchezo wakiwa uwanjani huku akiwataka wahakikishe wanapata bao mapema ili kuuweka mchezo kuwa mgumu kwa wenyeji.
    “Kwa hali hiyo sisi tunauhakika kabisa Azam FC wapo katika nafasi nzuri ya kupita na mambo mengine tunamwachia Mungu, cha msingi wachezaji wa Azam FC wawe na nidhamu ya mchezo ya kujua kuwa wanacheza ugenini na nadhani mwalimu atakuwa amelichukulia uzito, Azam FC sio wageni kwenye michuano ya kimataifa, karibu wanamiaka mine sasa wanashiriki na makosa waliyojifunza nyuma huko watayarekebisha ili waweze kupita,” alimalizia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BALOZI WA AFRIKA KUSINI AISIFU AZAM, KIGOGO WA TFF AITABIRIA USHINDI SWAZILAND Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top