TIMU ya Mtibwa Sugar imeibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya KMC FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara mchana wa leo Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Mabao ya Mtibwa Sugar yamefungwa na Frederick Magata dakika ya 31, Oscar Masai dakika ya 45, Said Mkopi dakika ya 48 na Kassim Msafiri dakika ya 53, wakati ya KMC FC yamefungwa na Daruwesh Saliboko kwa penalti dakika ya 51, Rashid Chambo dakika ya 57 na Adam Uledi dakika ya 58.
Kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar inafikisha pointi 26 na kusogea nafasi ya 10, ikiishushia nafasi ya 11 Fountain Gate FC yenye pointi 25 baada ya hizo zote kucheza mechi 23.
Hali inazidi kuwa mbaya kwa KMC baada ya kupoteza mchezo wa leo ikiendelea kushika mkia kufuatia kuvuna pointi tisa tu katika mechi 23 ilizocheza hadi sasa kwenye ligi ya timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja na mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment