TIMU ya Dodoma Jiji imetoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Airtel Mwigulu mjini Singida.
Hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa 2-1, mabao yake yote yakifungwa na kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Uganda, Allan Jolly Okellon ‘Star Boy’ dakika ya pili na 41, huku la Dodoma Jiji FC akijifunga beki na Nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto dakika ya 29.
Mambo yakageuka kipindi cha pili baada ya watokea benchi, winga Dickson Isaac Ambundo na mshambuliaji Waziri Junior Shentembo kwenda kutumia uzoefu wao kupindua meza dhidi ya timu yao ya zamani.
Kiungo Mwana Kibuta David aliifungia Dodoma Jiji FC bao la kusawazisha dakika ya 90, kabla ya Waziri Junior kufunga la ushindi dakika ya 90’+6 wote wakimfunga kipa Hussein Masalanga aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya kipa namba moja, Djigui Diarra raia wa Mali wakati Yanga inaongoza 2-1.
Kwa ushindi huo, Dodoma Jiji wanafikisha pointi 32 na kusogea nafasi ya saba, nyuma ya TRA United yenye pointi 34 na JKT Tanzania pointi 36 katika nafasi ya sita na tano baada ya timu zote kucheza mechi 23.
Kwa upande wao Yanga SC baada ya kupoteza mchezo huo wa kwanza wa msimu wanabaki na pointi zao 54 za mechi 23 sasa, ingawa wanaendelea kuongoza Ligi Kuu wakifuatiwa na watani wao, Simba SC wenye pointi 49 za mechi 22 na kesho watakuwa Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma katika mchezo wa 23 wa msimu dhidi ya wenyeji, Mashujaa FC.



.png)
0 comments:
Post a Comment