• HABARI MPYA

    Tuesday, January 24, 2017

    TFF YAUFUNGIA UWANJA WA JAMHURI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeufungia Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ili kutoa fursa kwa wamiliki wake kuufanya marekebisho makubwa kwenye eneo la kuchezea mpira.
    Taarifa ya TFF leo imesema kwamba Uwanja umesimamishwa kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ili pamoja na kuwapa fursa wamiliki wake kuukarabari, lakini pia askari polisi kupata maelekezo ya kutosha ya jinsi ya kusimamia usalama uwanjani badala ya kutazama mechi. 
    TFF imesema kama marekebisho hayatafanyika, Uwanja huo hautatumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
    Na hatua hiyo inafuatia mashabiki kuingia uwanjani baada ya mechi namba 151 baina ya wenyeji, Mtibwa Sugar na Simba. 
    TFF imesema baada ya mchezo kumalizika mashabiki waliingia uwanjani kwa wingi na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wachezaji, waamuzi na waandishi wa habari. "Pia kamera ya Azam Tv upande wa goli la Kusini iliangushwa na washabiki hao.Vilevile sehemu ya kuchezea (pitch) ya Uwanja wa Jamhuri iko katika hali mbaya ambapo inahitaji marekebisho makubwa ili iweze kuendelea kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom,".
    "TFF imebaini kuwa kitendo cha washabiki kuingia uwanjani baada ya filimbi ya mwisho, licha ya kuwa ni kinyume cha kanuni lakini pia kilichangiwa na askari polisi kutokuwa makini katika majukumu yao ya kusimamia usalama uwanjani na badala yake kuelekeza umakini katika kutazama mechi,".
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAUFUNGIA UWANJA WA JAMHURI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top