• HABARI MPYA

    Wednesday, January 25, 2017

    HANS POPPE: HATUTAINGIA KICHWA KICHWA KWA OKWI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imesema kwamba italazimika kujiridhisha kwanza juu ya kiwango cha mshambuliaji wake wa zamani, Emmanueo Arnold Okwi kabla ya kuamua kumsajili tena.
    Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe alipozungumza na Bin Zubeiry Sports- Online leo mjini Dar es Salaam. 
    Okwi aliyezaliwa Desemba 25, mwaka 1992 amevunja mkataba na klabu ya Sonderjyske ya Denmark aliyojiunga nayo Julai mwaka juzi, baada ya kuona hapati nafasi ya kucheza.
    Na Hans Poppe alisema jana kwamba kwa sababu Okwi ameondoka kwenye klabu hiyo akiwa hachezi, Kamati ya Ufundi italazimika kujiridhisha kwanza kuhusu kiwango chake.
    Hans Poppe (kulia) akimkabidhi jezi Okwi baada ya kumsajili tena akitokea Yanga mwaka juzi

    “Okwi ni mchezaji wetu na Simba ni nyumbani kwake. Milango ipo wazi kwake kurejea, lakini litakapofika suala la kusajiliwa tena, lazima Kamati ya Ufundi ijiridhishe kuhusu kiwango chake,”alisema Hans Poppe. 
    Okwi alijiunga na SonderjyskE FC ya Ligi Kuu ya Denmark Julai mwaka 2015 akisaini mkataba wa miaka mitano kutoka Simba SC, ambao ulitarajiwa kumalizika mwaka 2020.
    Okwi aliyeifungia mabao 18 timu ya taifa ya Uganda katika mechi 35, aliondoak Simba SC baada ya nusu msimu tu tangu arejee kutokea kwa mahasimu, Yanga SC ambako pia alicheza kwa nusu mwaka kabla ya kutofautiana na viongozi wa klabu hiyo na kuondoka.
    Simba SC ndiyo iliyomuingiza Tanzania Okwi mwaka 2010 akitokea SC Villa ya kwao. Alicheza Msimbazi hadi mwaka 2013 aliponunuliwa na Etoile du Sahel ya Tunisia kwa dola za KImarekani 300,000 (Sh. Milioni 600 na zaidi).
    Hata hivyo, Okwi aliondoka Tunisia baada ya miezi mitatu kufuatia kutofautiana na uongozi wa klabu hiyo na baadaye kufungua kesi FIFA akiomba aruhusiwe kucheza klabu nyingine kulinda kipaji chake wakati mgogoro wake na Etoile unaendelea.
    Etoile ilisitisha huduma kwa Okwi, baada ya kukerwa na desturi ya mchezaji huyo kuchelewa kurejea kujiunga na timu anaporuhusiwa kwenda kujiunga na timu yake ya taifa Uganda.
    Akasaini tena SC Villa katikati ya mwaka 2013 kabla ya Desemba mwaka huo, kuhamia Yanga SC- wakati wote huo kesi yake na Etoile ikiendelea FIFA. 
    Hata hivyo, Agosti mwaka jana, Okwi akarejea Simba SC kwa Mkataba wa miaka miwili kabla ya mwezi huu kuhamia Denmark. 
    Etoile haikuwahi kuilipa Simba SC fedha za manunuzi ya Okwi na klabu ya Tanzania ilifungua kesi FIFA ikashinda na kulipwa mwaka jana wakati imekwishamuuza tena Okwi Denmark.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE: HATUTAINGIA KICHWA KICHWA KWA OKWI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top