• HABARI MPYA

  Jumatatu, Januari 23, 2017

  AZAM NAYO YAENDA 16 BORA KOMBE LA SHIRIKISHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imeitoa Cosmopolitan katika michuano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa kuifunga mabao 3-1 jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo kwenye mchezo wa Raundi ya Tano, Azam FC inaungana na vigogo Simba na Yanga kwenda hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo. 
  Yanga iliitoa Ashanti United kwa mabao 4-1 Jumamosi wakati Simba jana iliitoa Polisi Dar kwa mabao 2-0, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. 
  Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ alifungua biashara nzuri dakika ya 69 kwa kuifunga timu iliyomuibua kisoka, Cosmo lakini hakushangilia bao hilo kuashiria heshima kwa timu yake ya zamani.
  Kinda Shaaban Iddi akaifungia bao la pili Azam dakika ya 76 kabla ya Cosmo kupata la kufutia machozi dakika ya 78 mfungaji Fidelis Kyanga na Joseph Mahundi kuifungia la tatu Azam dakika ya 80.
  Baada ya mchezo huo, Azam FC inakwenda kambini kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba SC Jumamosi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.   
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk73, Himid Mao, Frank Domayo, John Bocco, Yahya Mohammed na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
  Cosmopolitan; George Kijombi, Ramadhan Yusuph, Maulid Jumanne, Abdul Kussy, Fidelis Kyangu, Salum Hamisi, Hassan Mussa/Hafidh Hamisi dk62, Omary Hamisi, Ally Kabunda, Nuru Thabit na Fakhi Rashid.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM NAYO YAENDA 16 BORA KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top