• HABARI MPYA

  Ijumaa, Januari 27, 2017

  SIMBA NA AZAM KUPIGWA UWANJA WA TAIFA KESHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SERIKALI imeufungulia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na imeruhusu mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Azam FC na Simba uchezwe hapo kesho.
  Simba watakuwa wenyeji wa Azam FC kesho katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mchezo huo sasa utafanyika Uwanja wa Taifa, badala ya Uhuru, Dar es Salaam kufuatia tamko la Serikali .
  Taarifa ya Zawadi Msalla, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali leo imesema kwamba Uwanja unafunguliwa baada ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kujiridhisha na ukarabati uliofanywa baada ya uharibifu uliosababishwa na tukio la Oktoba 1, mwaka huu.
  Siku hiyo kulitokea vurugu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baina ya mahasimu, Simba na Yanga hadi kuvunja viti.
  Mashabiki wa Simba walifanya vurugu Uwanja wa Taifa Oktoba 1, mwaka huu baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu.
  Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
  Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.
  Katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
  Na mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani.
  Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
  Oktoba 2, Wizari ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, ikasema Rais kwamba Magufuli alikuwa anautazama mchezo huo moja kwa moja kupitia Azam TV na akajionea mwenyewe vurugu na chanzo chake.
  Ikasema Rais Magufuli alikasirika mno na akataka hatua kali zichukuliwe, lakini akamtuliza na mwishowe hatua iliyochukuliwa ni kuzizuia timu hizo kutumia Uwanja huo.  
  Aidha, Serikali pia ikazuia mapato ya mchezo huo hadi hapo itakapokata gharama za uharibifu uliosababishwa na vurugu hizo. 
  Lakini leo, ikiwa ni zaidi ya siku 100 tangu Uwanja ufungiwe, Serikali inarudi nyuma na kuufungulia na sasa Azam na Simba zitamenyana Taifa kesho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA NA AZAM KUPIGWA UWANJA WA TAIFA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top