• HABARI MPYA

    Tuesday, January 31, 2017

    MKWASA KATIBU MKUU MPYA YANGA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MCHEZAJI na kocha wa zamani wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa leo ametambulishwa rasmi kuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, akichukua nafasi ya Baraka Deusdedit anayerejea kwenye Idara yake ya Fedha.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema kwamba Mkwasa anaanza majukumu yake rasmi Februari 1, mwaka huu.
    Sanga alisema kuwa sababu kubwa ya kumchagua Mkwasa ni kuhimarisha safu ya uongozi wa klabu hiyo  ambapo aliyekuwa kaimu katibu mkuu, Baraka Deusdedit anarejea katika nafasi yake ya zamani ya Ukurugenzi wa Fedha.
    Charles Boniface Mkwasa sasa ndiye Katibu Mkuu wa Yanga na Baraka Deusdedit anarejea kwenye Idara yake ya Fedha

    “Najua wadau wa soka wanajiuliza kwa nini Mkwasa ameshika nafasi hiyo ya Ukatibu Mkuu kwa sabab ya taaluma yake inayojulikana ni ufundisha mpira wa miguu, siyo kweli, Mkwasa anauzoefu mkubwa katika kazi hiyo tofauti na watu wanavyomuelewa,”
    “Na hii si mara ya kwanza, hata Zambia, Kalusha Bwalya amewahi kuwa katibu mkuu wa chama cha soka nchini humu huku wakijua kuwa ni mchezaji mstaafu au kocha, Yanga tumemuona Mkwasa ni bora ya zaidi katika nafasi hiyo,” alisema Sanga.
    Mkwasa alishukuru kushika nafasi hiyo na kuahidi kuifikisha Yanga katika malengo yaliyowekwa. “Naomba nieleweke wazi kuwa mimi ni Katibu Mkuu wa Yanga na wala siyo kocha, najua kuna watu watafikiria kuwa narejea kwa mlango wa nyuma, kamwe sitaingilia masuala yoyote ya ufundi zaidi ya kufanya yale yaliyomo katika majukumu yangu,” alisema Mkwasa.
    “Ninaomba ushirikiano kutoka kwa wanachama, mashabiki, viongozi wenzangu, sisi sote tupo hapa Yanga kwa ajili ya kuiletea maendeleo na si vinginevyo,” alisema.
    Na Mkwasa anarejea Yanga ndani ya mwezi mmoja tangu aondolewe timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na nafasi yake kupewa Salum Mayanga.
    Mkwasa aliifundisha Taifa Stars tangu Julai mwaka 2015 baada ya kurithi nafasi ya Mholanzi, Mart Nooij na katika kipindi chake aliiongoza timu hiyo katika mechi 13, ikishinda mbili, kufungwa sita na sare tano.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKWASA KATIBU MKUU MPYA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top