• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 25, 2017

  IVORY COAST WAVULIWA UBINGWA AFCON

  IVORY Coast wamevuliwa ubingwa wa Afrika baada ya kufungwa 1-0 na Morocco, bao pekee la Rachid Alioui likimuinua kocha Mfaransa Herve Renard katika mchezo wa Kundi C Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Gabon.
  Ushindi huo unaompeleka Robo Fainali ni faraja kwa kocha Renard, ambaye miaka miwili iliyopita alikuwa akiifundisha Ivory Coast.
  Kocha huyo mwenye umri wa miaka 48, akiwa amevalia shati yake ya bahati nyeupe, anatumai kuwa kocha wa kwanza kushinda mataji matatu ya AFCON na timu tatu tofauti, baada ya awali kufanya hivyo akiwa na Zambia na Ivory Coast.
  Mshambuliaji wa Ivory Coast, Wilfred Zaha (kuliua) akipambana na kiungo wa Morocco, Nabil Dirar katika mchezo wa Kundi C jana 

  Aliipa taji hilo Zambia mwaka 2012 na akarudia akiwa na Ivory Coast miaka mitatu baadaye.
  Bao hilo pekee la ushindi lilipatikana dakika ya 64 kutoka kwa mchezaji anayecheza Ufaransa, Alioui na sasa watakutana na washindi wa Kundi D katika Robo Fainali mjini Port-Gentil Jumapili.
  Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo (DRC) iliifunga Togo 3-1 kwenye mchezo mwingine wa Kundi C na kuongoza kundi hilo kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na Morocco pointi sita, Ivory Coast mbili na Togo moja.
  Mabao ya DRC jana yalifungwa na Junior Kabananga dakika ya 29, Firmino Mubele dakika ya 54 na Paul-Jose 'M'Poku dakika ya 80, wakati la Togo lilifungwa na Kodjo Fo-Doh Laba dakika ya 69.
  Hatua ya makundi itahitimishwa leo kwa mechi za Kundi D kati ya Uganda na Mali Uwanja wa d'Oyem na Misri na Ghana Uwanja wa Port Gentil, mechi zote zikianza Saa 4:00. 
  Ghana inaongoza Kundi hilo kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Misri yenye pointi nne, Mali pointi moja na Uganda haina pointi.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: IVORY COAST WAVULIWA UBINGWA AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top