• HABARI MPYA

  Jumamosi, Januari 28, 2017

  BOSSOU AREJEA KUONGEZA NGUVU YANGA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imesema inamtarajia beki wake tegemeo, Vincent Bossou kurejea nchini kuanzia kesho baada ya kukosekana mwezi wote huu akiwa na timu yake ya taifa, Togo kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
  Kaimu Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit aliiambia Bin Zubeiry Sports - Online jana kwamba wanatarajia Bossou atawasili wakati wowote kuanzia Jumapili baada ya Togo kutolewa AFCON.
  “Kwa kweli matarajio yetu atakuwa hapa kuanzia Jumapili, kwa sababu kule timu yake imetolewa na anafahamu anatakiwa kurejea hapa haraka kuendelea na majukumu yake,”aliseam Baraka.
  Vincent Bossou anatarajiwa kurejea nchini kuanzia kesho baada ya Togo kutolewa kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Gabon

  Bossou alikuwa nchini Gabon kwenye AFCON, ambako kwa bahati mbaya timu yake, Togo imetolewa baada ya hatua ya makundi tu kufuatia kuambulia pointi moja tu baada ya mechi za tatu za Kundi A.
  Ilifungwa 3-1 mara mbili na Morocco na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kutoa sare ya 0-0 na Ivory Coast na kwa bahati mbaya mechi zote hizo Bossou alikuwa benchi hakucheza.  
  Wachezaji wengine wa Ligi Kuu ya Bara waliokuwa AFCON ni beki wa Simba, Juuko Murshid aliyekuwa na kikosi cha Uganda na winga Bruce Kangwa wa Azam FC aliyekuwa na Zimbabwe, ambao wote timu zao hazikuvuta hatua ya makundi.
  Zimbawe walishika mkia Kundi C wakiambulia pointi moja baada ya kufungwa mechi mbili na sare moja, sawa na Uganda walioshika mkia Kundi D pia kwa kuambulia pointi moja baada ya sare moja na kufungwa mechi mbili. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BOSSOU AREJEA KUONGEZA NGUVU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top