• HABARI MPYA

    Saturday, January 28, 2017

    NI AZAM TENA, AU SIMBA KUNG'ARA LEO TAIFA?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa nyasi za viwanja vinne kuhimili patashika ya miamba nane.
    Lakini patashika ambayo inatarajiwa kuvutia hisia za wengi ni kati ya vinara wa ligi hiyo, Simba SC dhidi ya Azam FC ambayo itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Timu hizo zinakutana tena leo ikiwa ni kiasi cha wiki mbili tangu zimenyane kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi na bao pekee la Himid Mao kwa shuti la mbali likaipa Azam ushindi wa 1-0 Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Kwa Azam ushindi huo ulikuwa sawa na kulipa kisasi cha kipigo kama hicho cha 1-0 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Septemba 17, mwaka jana Uwanja Uhuru, Dar es Salaam bao pekee la Shiza Kichuya.
    Baada ya kila timu kushinda mechi moja katika michezo miwili iliyozikutanisha timu hizo msimu huu, leo zinakutana kwa mara ya tatu na ya mwisho labda katika msimu huu.
    Mchezo wa leo unatarajiwa kuchezeshwa na refa Erick Onoka atakayesaidiwa na washika vibendera Hassan Zani, wote wa Arusha na Josephat Masija wa Mwanza, wakati mezani atakuwapo Soud Lila wa Dar es Salaam na Kamisaa ni Michael Bundala wa.
    Mchezo wa leo ni muhimu zaidi kwa Simba kushinda, wao ndiyo wapo kwenye mbio za ubingwa wakifukuziwa kwa karibu mno na mahasimu wao wa jadi, Yanga SC.
    Simba SC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 45 ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 43 baada ya kila timu kucheza mechi 19.
    Ushidi katika mchezo wa leo kwa Simba, inayofundishwa na kocha Mcameroon, Joseph Omog utawahakikishia kumaliza wikiendi hii wakiwa kileleni hata kama Yanga itashinda dhidi ya Mwadui FC kesho.
    Lakini kwa Azam FC, kocha mpya Mromania, Aristica Cioaba atahitaji kuwa na mwanzo mzuri kwa kuhakikisha anashinda leo – na ndiyo maana mchezo wa leo utakuwa mtamu.
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo ni kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Toto Africans na African Lyon Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Ndanda FC na Maji Maji Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
    Kesho mabingwa watetezi,  Yanga watamenyana na Mwadui FC Uwanja wa Taifa na keshokutwa Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba na JKT Ruvu wataikaribisha Stand United Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI AZAM TENA, AU SIMBA KUNG'ARA LEO TAIFA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top