• HABARI MPYA

  Jumapili, Januari 29, 2017

  OMOG ASITOLEWE KAFARA SIMBA SC

  SIMBA SC jana imefungwa 1-0 na Azam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Shujaa wa Azam jana alikuwa Nahodha wake, John Raphael Bocco aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 70 baada ya makosa ya beki, Method Mwanjali kutaka ‘kuuremba’ mpira kwenye eneo la hatari.  
  Bocco aliupitia mpira miguuni mwa Mwanjali na kwenda kumfunga kipa Mghana, Daniel Agyei. Kunzia hapo, Uwanja wa Taifa ukawa kimya. 
  Hicho kinakuwa kipigo cha pili mfululizo ndani ya mwezi mmoja Simba wanapewa na Azam, baada ya Januari 13 kufungwa pia 1-0 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan, Zanzibar, bao pekee la Himid Mao.
  Baada ya mchezo huo lawama zimeanza kuelekezwa kwa kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog kwamba yeye ndiye ameiponza timu kufungwa.
  Na mbaya zaidi lawama zinatoka kwa ‘watu wazito’ ndani ya Simba, maana yake hatua zinaweza kuchukuliwa.
  Na ukizingatia rekodi za Simba kufukuza makocha baada ya muda mfupi kwa misimu ya karibuni kwa namna yoyote huwezi kupuuza vuguvugu hili.
  Ni kwamba Omog amekalia kuti kavu kwa sasa Simba, wenyewe wakiamini walikosea kumchukua kocha huyo wa zamani wa Azam FC.
  Hakuna kingine kinachomuweka matatani kwa sasa Omog zaidi ya matokeo. 
  Timu haikuchukua Kombe la Mapinduzi ikifungwa na Azam 1-0, ikaenda kulazimishwa sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar Uwanja mgumu wa Jamhuri, Morogoro, ikapata ushindi mwembamba dhidi ya Polisi Dar kwenye Kombe la Shirikisho Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) kabla ya kipigo cha juzi.
  Mwanzoni tu mwa msimu wakati wanamleta Omog, Simba walijinasibu kwamba msimu huu watachukua ubingwa baada ya kuukosa tangu mwaka 2012.
  Simba walitumia vizuri fedha za mauzo ya mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi dola za Kimarekani 300,000 kutoka Etoile du Sahel ya Tunisia kwa kusajili wachezaji wengi wapya wa kiwango cha juu.
  Iliibomoa himaya ya Mtibwa Sugar na kuwachukua viungo Muzamil Yassin, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim na Shiza Kichuya – ikawasajili pia Hamad Juma, Jamal Mnyate, Emmanuel Semwanza na Malika Ndeule kwa upande wa wazawa. Ilimsajili pia mshambuliaji Ame Ali kwa mkopo kutoka Azam, ambaye baada ya nusu msimu ikamtema sasa hivi yupo Kagera Sugar.
  Kwa wageni iliwasajili mabeki Janvier Bokungu kutoka DRC, Mwanjali, kiungo Mussa Ndusha wa DRC, washambuliaji Laudit Mavugo wa Burundi na Frederick Blagnon wa Ivory Coast.
  Simba ikawa na mzunguko mzuri wa kwanza wa Ligi Kuu ikimalizia kileleni, lakini wakati wa dirisha dogo ikaboresha kikosi.
  Ikawatema kipa Muivory Coast, Vincent Angban na kiungo Mkongo Ndusha upande wa wachezaji wa kigeni na kuwasajili Waghana kipa Agyei na kiungo James Kotei pamoja na wazawa, washambuliaji Pastory Athanas kutoka Stand United na Juma Luizio kutoka Zesco United kwa mkopo.
  Kwa upande wa wazawa ikamtema Ndeule na kumtoa kwa mkopo Semwanza kwenda Maji Maji ya Songea.
  Baada ya kurejea kutoka kwenye Kombe la Mapinduzi, Simba ikamtoa kwa mkopo Blagnon kwenda Oman Club.
  Huyo ni mchezaji ghali zaidi katika kikosi cha Simba msimu huu, akisajiliwa kwa dau la dola za Kimarekani 50,000 (zaidi ya Sh. Milioni 100) na kulipwa mshahara wa dola 3,000 (zaidi ya Sh. Milioni 6).
  Ni mshambuliaji ambaye Simba iliweka matumaini makubwa sana kwake, sasa ameondoka baada ya kushindwa kuonyesha thamani yake klabuni.
  Hayo mambo yanatokea hadi Ulaya, anasajiliwa mchezaji kwa matumaini makubwa, lakini anashindwa kutimiza ndoto – si ajabu kwa Simba.
  Mshambuliaji mwingine tegemeo aliyesajiliwa Simba msimu huu, Laudit Mavugo kwa muda mwingi amekuwa akitokea benchi.
  Na mshambuliaji aliyemaliza msimu uliopita akiwa tegemeo la timu, Ibrahim Hajib msimu huu matumizi yake yamepungua uwanjani.
  Amekuwa akitokea benchi zaidi na nafasi yake imezidi kupungua baada ya ujio wa Luizio na Athanas.
  Kwa tafsiri ya haraka haraka ni kwamba mipango ya Simba imefeli. Blagnon hakukidhi mahitaji na bahati mbaya hata Shiza Kichuya aliyekuwa tegemeo la mabao mzunguko wa kwanza, amepoteza makali.
  Jana Kichuya alianzishiwa benchi na alipoingia kipindi cha pili akaenda kupiga krosi moja nzuri iliyounganishwa kwa kichwa na kuokolewa kwa ustadi mkubwa na kipa wa Azam, Aishi Manula.
  Kuanza kumsukumia lawama Omog kwa sasa si sahihi, kwa sababu kinachoonekana kwa mapana marefu ni kufeli kwa mipango ya klabu.
  Imeonekana Omog anapenda mfumo wa kutumia mshambuliaji mmoja na viungo wengi – hivyo kama anakosa mtu aina ya Blagnon wazi atakwama sehemu katika mipango yake.
  Kwa muda mrefu Simba imekuwa ikiona suluhisho ni kufukuza makocha, lakini nadhani wakati umefika sasa watafute suluhisho mbadala.
  Hata Manchester United ya England baada ya kufukuza makocha mfululizo na kila iliyemleta akawa na mwanzo mbaya, akiwemo wa sasa Jose Mourinho, mwishowe imeamua kutulia na Mreno huyo na sasa mambo yanaanza kunyooka taratibu.  
  Inawezekana kweli Omog akawa tatizo, lakini vyema Simba ikajipa muda hadi mwisho wa msimu kabla ya kuchukua hatua yoyote.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: OMOG ASITOLEWE KAFARA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top