• HABARI MPYA

  Ijumaa, Januari 27, 2017

  WAZUNGU WAMUOMBEA ITC ULIMWENGU AANZE KAZI SWEDEN

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya AFC Eskilstuna ya Ligi Kuu ya Sweden imemuombea Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu tayari kuanza kumtumia baada ya kumsajili.
  Tangu juzi Ulimwengu yuko Hispania na klabu yake hiyo mpya, AFC Eskilstuna kwa maandalizi ya Ligi Kuu ya Sweden. 
  Na akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema kwamba AFC Eskilstuna imekwishaomba ITC ya Ulimwengu. “Tayari tumepokea maombi ya ITC ya Ulimwengu kutoka klabu ya AFC Eskilstuna,”alisema Lucas. 
  AFC Eskilstuna imemuombea ITC Thomas Ulimwengu ili ianze kumtumia katika Ligi ya Sweden

  Ulimwengu amesaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, ambayo awali ilikuwa inajulikana kama FC Cafe Opera na Vasby United akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya Athletic FC ya Sweden, alikocheza hadi 2011 TP Mazembe alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
  Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
  Ulimwengu anajivunia kushinda mataji makubwa akiwa na  Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WAZUNGU WAMUOMBEA ITC ULIMWENGU AANZE KAZI SWEDEN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top