• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 25, 2017

  YANGA KUENDELEA KUWAKOSA ZULU, NGOMA DHIDI YA MWADUI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC itaendelea kuwakosa wachezaji wake wawili wa kigeni, kiungo Justin Zulu na mshambuliaji Donald Ngoma katika mechi yake ya wikiendi hii.
  Yanga SC watakuwa wenyeji wa Mwadui FC ya Shinyanga Jumapili katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mjini Dar es Salaam.
  Na kuelekea mchezo huo, Kaimu Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit aliiambia Bin Zubeiry Sports - Online jana kwamba timu itaendelea kuwakosa kiungo Mzambia, Zulu na mshambuliaji Mzimbabwe Ngoma.
  Kiungo Justin Zulu (kushoto) akiwa na Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' (kulia)

  Baraka alisema kwamba Zulu bado majeruhi na Ngoma pamoja na kwamba bado majeruhi pia, lakini aligtarajiwa kurejea jana kutoka kwao, Zimbabwe alipokwenda kwenye msiba wa ndugu yake. 
  “Wachezaji wote wapo kambini kwa maandalizi ya mchezo wetu wa wikiendi dhidi ya Mwadui, kasoro Zulu na Ngoma ambao ni majeruhi. Ngoma pamoja na kuwa majeruhi, lakini pia alifiwa na alikwenda kwao Zimbabwe kuzika,”alisema Baraka.
  Tayari Yanga SC imeandika barua Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kuomba mechi zake zote zijazo kuanzia na Mwadui zihamishiwe Uwanja wa Taifa ambako wameruhusiwa kucheza mechi za michuano ya Afrika pekee. 
  Na sababu za Yanga kuomba hivyo ni kwamba mwezi ujao wanaanza kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo ni vyema wakaanza kuchezea Uwanja wa Taifa ili wauzoee.     
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA KUENDELEA KUWAKOSA ZULU, NGOMA DHIDI YA MWADUI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top