• HABARI MPYA

  Jumatatu, Januari 30, 2017

  YANGA SC WAKATAA KUCHEZA NA MAMELODI SUNDOWNS

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imekataa kucheza na mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundwons ya Afrika Kusini Ijumaa wiki hii kwa madai eti kocha wake, Mzambia George Lwandamina amekataa.
  Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit ameiambia Bin Zubeiry Sports - Online leo kwamba kocha Lwandamina amekataa mchezo dhidi ya Mamelodi uliokuwa ufanyike kwa kuwa unaingilia programu zake.
  “Hatutacheza na Mamelodi kwa sababu kocha ameukataa huo mchezo, amesema unaingilia programu zake, kama unavyojua kwa sasa tupo kwenye hatua ngumu ya Ligi Kuu na wakati huo huo tunaingia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika,”alisema.
  Yanga imesema kocha wake, Mzambia George Lwandamina amekataa mechi na Mamelodi

  Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Mwadui FC, Yanga SC itamenyana na timu nyingine ya Shinyanga Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu.
  Na Deusdedit alisema jana kwamba kocha amesema hawezi kuingia kwenye mchezo na Stand United siku mbili baada ya kucheza Mamelodi.  
  Kwa upande wake, waandaaji wa mechi hiyo pamoja na kusikitishwa na kitendo cha Yanga kugomea mchezo huo, lakini tayari wameiteua Azam FC kuchukua nafasi hiyo.
  Sasa Memelodi baada ya kucheza na Simba Jumatano wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam watahamia Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Ijumaa kucheza na Azam.
  Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini walitarajiwa kuwasili nchini jana kwa ziara ya michezo miwili ya kirafiki.
  Timu hiyo maarufu kama ‘Wabrazil’ kutokana na kuvalia jezi za njano kama timu ya taifa ya Brazil, inakuja nchini kwa mwaliko wa klabu ya African Lyon ya Dar es Salaam.
  Mkurugenzi wa African Lyon, Rahim Kangenzi ‘Zamuda’ alisema Mamelodi wanakuja nchini kushiriki kampeni ya kupiga vita ujangili, iitwayo Linda Tembo Wetu.  
  Na Zamunda amesema timu hiyo  ya mjini Pretoria itakuwa nchini kwa wiki yote ya kwanza Februari kushiriki kampeni hiyo pamoja na kucheza mechi hizo.
  Kuhusu kujiondoa kwa Yanga, Zamunda alisema kwamba hawana cha kufanya zaidi ya kukubaliana nao, lakini amesikitishwa na hilo.
  “Tulikwishazungumza na Yanga na tukakubaliana watacheza, tena wakatupa masharti kwamba tuwape kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya safari yao ya kwenda Comoro na kurudi kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika na tukawakubalia,”alisema Zamunda.
  Timu hiyo ya bilionea wa madini Afrika Kusini, Patrice Motsepe kwa hapa nchini kwenye mechi za mashindano imewahi kucheza Yanga SC pekee katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001.
  Ilikuwa ni katika hatua ya 16 Bora kwenye Ligi ya Mabingwa na Yanga ikatolewa kwa jumla ya mabao 6-5 baada ya kufungwa 3-2 Pretoria Mei 13 na kulazimishwa sare ya 3-3 Mei 26 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WAKATAA KUCHEZA NA MAMELODI SUNDOWNS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top