• HABARI MPYA

    Tuesday, January 24, 2017

    REFA WA YANGA NA MAJIMAJI AFUNGIWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limemwondoa Mwamuzi Hussein Athuman kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) baada ya kupata alama za chini ambazo hazimwezeshi kuendelea tena kuchezesha Ligi hiyo.
    Mwamuzi Hussein Athuman kutoka Mkoa wa Katavi alichezesha mchezo namba 150 uliozikutanisha timu za Majimaji ya Songea na Yanga ya Dar es Salaam, kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
    Kadhalika Yanga imepigwa faini ya jumla ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na timu yao kutoingia vyumbani, na pia kutumia mlango usio rasmi wakati wa kuingia uwanjani, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14 (13) na (14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.
    Mwamuzi Ngole Mwangole: Mwamuzi huyo wa kati, Ngole Mwangole wa Mbeya amepewa barua ya onyo kali na kumtaka aongeze umakini wakati akichezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kubainika kukataa bao lililoonekana kutokuwa na mushkeli la Mtibwa Sugar dhidi ya JKT Ruvu katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
    Licha ya kujitetea, lakini kamati haikuridhika na maelezo yake. Hata hivyo, kwa kuzingatia kuwa Mwangole alikuwa Mwamuzi Bora wa msimu uliopita (2015/2016) na hiyo ndiyo mara yake ya kwanza kuonekana kufanya uamuzi uliokosa umakini wakati akichezesha, TFF imeamua kumpa onyo.
    Mechi namba 141 (Mwadui FC vs Kagera Sugar). Beki wa Kagera Sugar, Godfrey Taita anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi baada ya mechi na kuwatolea lugha chafu na vitisho kabla ya benchi la ufundi la timu yake pamoja na askari polisi kuingilia kati na kudhibiti kadhia hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: REFA WA YANGA NA MAJIMAJI AFUNGIWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top