• HABARI MPYA

  Ijumaa, Januari 27, 2017

  MAMELODI KUTUA DAR JUMATATU KUCHEZA NA SIMBA,YANGA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MABINGWA wa Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini wanatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu kwa ziara ya michezo miwili ya kirafiki dhidi ya vigogo wa Tanzania, Simba na Yanga.
  Timu hiyo maarufu kama ‘Wabrazil’ kutokana na kuvalia jezi za njano kama timu ya taifa ya Brazil, inakuja nchini kwa mwaliko wa klabu ya African Lyon ya Dar es Salaam.
  Mkurugenzi wa African Lyon, Rahim Kangenzi ‘Zamuda’ ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Mamelodi wanakuja nchini kushiriki kampeni ya kupiga vita ujangili, iitwayo Linda Tembo Wetu.  
  Mamelodi Sundowns wanatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu

  Na Zamunda amesema timu hiyo  ya mjini Pretoria itakuwa nchini kwa wiki yote ya kwanza Februari kushiriki kampeni hiyo pamoja na kucheza mechi hizo.
  Alisema mchezo wa kwanza utachezwa Februari 1 na wa pili Februari 3 mwaka 2017 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ingawa hakusema itaanza kucheza na timu gani kati ya Simba na Yanga.
  Timu hiyo ya bilionea wa madini Afrika Kusini, Patrice Motsepe kwa hapa nchini kwenye mechi za mashindano imewahi kucheza Yanga SC pekee katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001.
  Ilikuwa ni katika hatua ya 16 Bora kwenye Ligi ya Mabingwa na Yanga ikatolewa kwa jumla ya mabao 6-5 baada ya kufungwa 3-2 Pretoria Mei 13 na kulazimishwa sare ya 3-3 Mei 26 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  Mkurugenzi wa African Lyon, Rahim Kangenzi 'Zamunda' (kushoto) akimkabidhi Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan fulana ya kampeni ya Linda Tembo Wetu
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAMELODI KUTUA DAR JUMATATU KUCHEZA NA SIMBA,YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top