• HABARI MPYA

  Jumapili, Januari 24, 2016

  KERR ‘AWAPASUA’ VIONGOZI WA SIMBA SC; AFICHUA MAMBO KIBAO IKIWEMO WACHEZAJI KUTOLIPWA MISHAHARA KWA WAKATI NA…

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  ALIYEKUWA kocha wa Simba SC, Muingereza Dylan Kerr amesema kwamba klabu hiyo haitafanikiwa bila kuajiri Mkurugenzi wa Ufundi, mwenye vyeti vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) au la Ulaya (UEFA).
  Katika taarifa yake kwa BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo, Kerr aliyefukuzwa wiki mbili zilizopita Simba SC, amesema kwamba Mkurugenzi wa Ufundi anayetambuliwa na CAF au UEFA ni muhimu katika klabu kwa ajili ya kufanya kazi kwa karibu na kocha.
  Amesema kwamba kwa sasa hali ilivyo ndani ya Simba shughuli nyingi za kiufundi zinafanywa kienyeji na watu ambao hawana taaluma hiyo, ambao ndiyo huajiri makocha, kusajili wachezaji na kufukuza pia.
  “Klabu haina hata Mjumbe mmoja wa bodi mwenye vyeti vya UEFA au CAF, ni hivi karibuni tu Mjumbe mmoja amekamilisha mafunzo ya awali ya ukocha kwa mara ya kwanza,”.
  Kocha Kerr (kushoto) amesema kwamba Simba SC inahitaji Mkkrugenzi wa Ufundi, ili mambo yaende sawa

  “Hadi klabu itakapomteua Mjumbe mmoja wa bodi mwenye sifa, anayetambuliwa na CAF au UEFA na mwenye uzoefu wa masuala ya soka, ili afanye kazi kwa karibu na kocha katika masuala kama ya usajili wa wachezaji, mipango ya mechi, mipango ya maandalizi ya kabla ya msimu, vifaa vya mazoezi, msingi wa soka la vijana na masuala yahusuyo soka kwa ujumla, ndipo itapiga hatua,”amesema.
  Amesema yeye si aina ya makocha waoga wa kupangiwa mambo na Wajumbe wa Bodi ambao hawana sifa, vigezo wala uzoefu wa masuala ya soka, ambao siyo tu wanataka kupanga timu (vikosi vya kucheza mechi), lakini pia kuwa na mamlaka ya kusajili na kufukuza wachezaji.
  Kerr pia amesema amepitia matatizo mengi Simba SC ambayo hakuwahi kusema katika kipindi chake cha kifupi cha kufanya kazi tangu Julai mwaka jana, ikiwemo yeye na wachezaji kucheleweshewa mishahara hususan mwezi Novemba na Desemba, lakini alivumilia. 
  Aidha, Kerr amelalamikia maombi yake juu ya masuala ya kitaalamu na kiufundi kutofanyiwa kazi na viongozi wa Simba SC, lakini baada ya kuondoka yakafanyiwa kazi.
  Amesema aliomba mipira halisi ya Addidas itumike katika mechi zao na si ile ya kiwango cha chini, ambayo wachezaji hawafurahii kuichezea, lakini hakusikilizwa.
  “Niliomba pia nyasi za Uwanja wa Taifa zipunguzwe, zilikuwa ndefu sana na kutuzuia kucheza vizuri kwa staili yetu. Sikutekelezewa. Ajabu sasa, baada ya mimi kuondoka, mipira halisi ya Addidas ndiyo inatumika katika mechi za Simba na nyasi za Uwanja wa Taifa zimepunguzwa,”amesema na kuongeza; “Bravo (hongera) Simba, lakini kwa nini sasa tu, niliomba kwa michezo 14 ya msimu, tuachane na hayo, hii ni kwa upande wangu, ninaweza kuwa mwisho wa matatizo,”amesema.
  Kuhusu kufukuzwa kwake baada ya timu kutolewa katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, Kerr amesema kwamba ni kinyume cha Mkataba wake wa miaka miwili na klabu.
  Kerr katikati akipongezwa na viongozi na wanachama wa Simba SC baada ya kufunga bao katika mechi ya viongozi wa klabu hiyo dhidi ya Wasanii kwenye tamasha la Simba Day Agosti mwaka jana 

  “Mkataba wangu wa miaka miwili, ulikuwa wazi kwamba nitahukumiwa kutoakana na matokeo ya Ligi Kuu mwishoni mwa msimu wa VPL wa 2015 - 2016 na matokeo yangu yalikuwa bado yananiweka katika nafasi ya kupata tiketi ya kucheza michuano ya Afrika mwaka 2017, tungefuzu,”amesema.
  “Naweza kuthibitisha hakuna kipengele kilichowekwa katika Mkataba wangu juu ya matokeo ya mechi za mashindano mengine au ile michuano ya Zanziba (Kombe la Mapinduzi) hivi karibuni,”.  
  “Niliamini kuwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, huku tukiendelea kupambana kupanda nafasi ya pili au ya kwanza, nilikuwa kwenye nafasi ya kutimiza matakwa niliyopewa na uongozi,”amesema.
  Amesema amesikitishwa timu kutolewa katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, lakini alitaka kuyatumia mashindano hayo kwa ajili ya kuwaandaa wachezaji kurejea kwenye ligi kwa ari na nguvu mpya ili waendelee kuwania ubingwa.
  Pamoja na yote, Kerr ameushukuru uongozi wa Simba SC, wachezaji na wapenzi kwa kipindi alichokuwa nao na kuwatakia heri chini ya zama mpya baada yeye kuondoka.
  Kwa sasa Simba SC ipo chini ya kocha Mganda, Jackson Mayanja ambaye mpango wa awali ilikuwa awe Msaidizi wa Kerr.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KERR ‘AWAPASUA’ VIONGOZI WA SIMBA SC; AFICHUA MAMBO KIBAO IKIWEMO WACHEZAJI KUTOLIPWA MISHAHARA KWA WAKATI NA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top