• HABARI MPYA

    Tuesday, January 19, 2016

    UHONDO LIGI KUU WAENDELEA; AZAM FC WAIENDEA MGAMBO, KIBADEN NA SIMBA…NA YANGA SC NA MAJIMAJI YA KALI ONGALA

    RATIBA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA…
    Januari 20, 2016
    JKT Ruvu Vs Simba SC
    Mgambo JKT Vs Azam FC
    Stand United Vs Toto Africans
    Ndanda FC Vs Mbeya City
    Prisons Vs Coastal Union
    Januari 21, 2016
    Yanga SC Vs Majimaji
    Mwadui FC Vs Kagera Sugar
    African Sports Vs Mtibwa Sugar
    Mchezaji tegemeo zaidi kwa sasa Simba SC, Ibrahim Hajib anaweza kukosekana kesho dhidi ya JKT Ruvu
    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea kesho na keshokutwa, huku mvuto zaidi ukiwa mechi za miamba watatu wanaofukuzana kileleni, Azam FC, Simba na Yanga SC.
    Yanga SC inaongoza Ligi Kuu kwa wastani wa mabao, ikiwa inalingana kwa pointi (36) na Azam FC iliyo nafasi ya pili, wakati Simba SC inafuatia ikiwa na pointi 30.
    Azam FC baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na vibonde African Sports Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam wanasafiri hadi Tanga kuwafuata Mgambo JKT.
    Mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua utafanyika kesho Uwanja wa Mkwakwani na Azam FC watahitaji ushindi ili kuendelea ‘kula sahani moja’ na Yanga SC katika mbio za ubingwa.
    Azam FC wanatarajiwa kuwa wageni wa Mgambo JKT kesho Uwanja wa Mkwakwani, Tanga

    Simba SC wao watakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho kumenyana na JKT Ruvu katika mchezo ambao utawakutanisha makocha wa zamani wa Kagera Sugar, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na Mganda Jackson Mayanja.
    Kibaden, kocha na mchezaji wa zamani wa Simba SC kwa sasa anaiongoza JKT Ruvu iliyofungwa 5-1 na Mgambo JKT, wakati Mayanja atakuwa kwenye mchezo wa pili tangu arithi mikoba ya Muingereza, Dylan Kerr Simba SC.
    Simba SC inaweza kumkosa mshambuliaji wake tegemeo, Ibrahim Hajib aliyeumia Jumamosi timu hiyo ikishinda 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mechi nyingine za Ligi Kuu kesho ni kati ya Stand United na Toto Africans Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Ndanda FC na Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Prisons dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Mabingwa watetezi, Yanga SC wao watashuka dimbani Alhamisi kumenyana na Majimaji ya Songea, iliyo chini ya kocha mpya, Muingereza mwenye asili ya Tanzania, Kalimangonga Sam Daniel Ongala.
    Yanga SC watakuwa wenyeji wa Majimaji FC Alhamisi Uwanja wa Taifa
    Kali Ongala, mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC na kocha Msaidizi wa zamani wa Azam FC, huo utakuwa mchezo wake wa pili tangu apewe timu hiyo, baada ya mwishoni mwa wiki kupata sare ya ugenini ya 1-1 na Coastal, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. 
    Na Yanga SC ambayo haikucheza soka ya kuvutia ikishinda 1-0 dhidi ya Ndanda mwishoni mwa wiki, itakutana na majaribu ya wachezaji wake wa zamani kesho, beki Lulanga Mapunda na mshambuliaji Danny Mrwanda ambao wapo Majimaji kwa sasa.
    Mechi nyingine za Ligi Kuu kesho ni kati ya Mwadui FC na Kagera Sugar Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na African Sports wataikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UHONDO LIGI KUU WAENDELEA; AZAM FC WAIENDEA MGAMBO, KIBADEN NA SIMBA…NA YANGA SC NA MAJIMAJI YA KALI ONGALA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top