• HABARI MPYA

  Jumapili, Januari 31, 2016

  RAIS MPYA CECAFA NAYE ‘HAAMBILIKI’?

  MICHUANO ya klabu barani Afrika itaanza katikati ya Februari, Yanga SC wakiifuata Cercle de Joachim nchini Mauritius kwa mchezo wa kwanza wa raundi ya Awali Februari 13, mwaka huu katika Ligi ya Mabingwa.
  Azam FC wataanzia ugenini Machi 11 
  dhidi ya mshindi kati ya Light Stars FC ya Shelisheli na Bidvest Wits ya Afrika Kusini katika Raundi ya Pili Kombe la Shirikisho.
  Na timu zote zitaingia katika michezo hiyo zikitokea katika ratiba ngumu ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, iliyoshika kasi katika mzunguko wake wa pili.
  Hali ambayo inasababisha majeruhi wengi na wachezaji kuchoka kwa mazoezi magumu ya kila siku na mechi mbili kwa wiki.

  Ni matarajio wiki moja kabla ya michezo yao, zitapewa mapumziko kwenye ligi ili waelekeze nguvu kwenye maandalizi ya mechi zao za Afrika.
  Nachotaka kuzungumzia leo ni kwa nini miaka ya nyuma, klabu zetu angalau zilikuwa zinasogea sogea mbele kwenye michuano ya Afrika, tofauti na sasa.
  Mwaka 1974 Simba SC iliingia katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika ikitokea katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, michuano ambayo waliibuka mabingwa mjini Dar es Salaam.
  Na katika Klabu Bingwa Afrika, Simba SC wakaenda hadi Nusu Fainali, ambako walitolewa na Mehallal El Kubra kwa penalti 3-0, bada ya sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
  Mwaka 1993 Simba SC waliingia kwenye michuano ya Kombe la CAF wakitokea kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mjini Kampala, Uganda.
  Bahati mbaya Simba SC ilishika nafasi ya tatu katika Kundi B nyuma ya Bata Bullets ya Malawi waliokuwa wa pili na wenyeji Express FC walioongoza Kundi, wakati El Hilal ya Sudan ilishika mkia.
  Na mwaka huo, wakafanikiwa kufika hadi Fainali ambako walifungwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast mabao 2-0 Dar es Salaam, baada ya sare ya 0-0 Abidjan.
  Mwaka 2003 Simba SC waliingia katika Ligi ya Mabingwa Afrika wakitokea katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, wakati huo tayari michuano imebadilishwa jina na kuwa Kombe la Kagame, ambako walifika fainali mjini Kampala Uganda na kufungwa na wenyeji SC Villa 1-0.    
  Na katika katika Ligi ya Mabingwa, Simba SC walifanikiwa kufika hatua ya makundi wakiitoa timu ngumu, Zamalek ya Misri ambao wakati huo ndiyo walikuwa mabingwa watetezi.
  Lakini baada ya hapo, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) likayumba na kujikuta linashindwa kuendelea kuendesha Kombe la Kagame katika muda wake.
  Michuano ya mwaka 2004 ilipangwa kufanyika mjini Kigali, Rwanda kama kawaida kuanzia Januari, lakini ikaahirishwa kwanza hadi Machi na baadaye hadi Aprili 25 hadi Mei 9, ili iende sambamba na maazimisho ya miaka 10 ya mauwaji ya Genocide mwaka 1994.
  Tangu hapo, michuano hiyo haikurudi katika muda wakati halisi Januari bali imeendelea kusogezwa mbele na sasa imefikia inafanyika Agosti tu.
  Agosti ni kipindi ambacho Ligi Kuu nyingi za ukanda huu ndiyo zinamalizika au zinaelekea kuanza, maana yake hata timu zinakuwa hazijawa vizuri kwa michuano.
  Lakini pia, imekuwa haina faida kufanya michuano hiyo Agosti kama ilivyokuwa awali ilipokuwa ikifanyika Januari, klabu zetu zilikuwa zikitoka kwenye Kagame zinaingia moja kwa moja kwenye michuano ya Afrika.
  Zilikuwa zinaingia kwenye michuano ya Afrika baada ya kupata vipimo vizuri katika Kombe la Kagame na haikuwa ajabu klabu zilizokuwa zinajipanga vizuri kama Simba SC ziliweza kufika mbali.
  Baada ya mwaka 2003 hakuna timu ya Tanzania iliyoweza kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika kwa sababu zimepoteza fursa nzuri ya kuitumikia michuano ya Kagame kama sehemu ya maandalizi yake. 
  Lakini pia, athari ni nyingi hadi kwenye michuano yenyewe, kwani imeshuhudiwa katika michuano ya mwaka jana mjini Dar es Salaam, waliokuwa mabingwa watetezi, El Merreikh ya Sudan wakishindwa kuja kwa sababu walikuwa kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Na hata washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Sudan, El Hilal nao hawakuja kwa sababu wapo kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika- badala yake wakaja washindi wa tatu na wa nne, Al Shandy na Khartoum.
  Hakuna ubishi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, klabu hizo mbili za Sudan zipo juu zaidi kisoka na hata kwa uwezo wa kujiendesha, tena kisasa kabisa.
  Kwa miaka ya karibuni imekuwa kawaida kwa timu stahiki kutojitokeza katika Kombe la Kagame kutokana na sababu za kawaida sana.
  Kwa mfano mwaka juzi, Yanga SC walitakiwa kusafiri hadi Rwanda, lakini wakagoma kwa sababu ndiyo kwanza walikuwa wanaanza maandalizi ya msimu mpya.
  Miaka ya nyuma, wakati mashindano haya yanafanyika Januari hakuna timu iliyostahili ilikuwa inakosekana.
  Timu nyingi zilichangamkia fursa ya kushiriki michuano hiyo, kwa sababu baada ya hapo zilikuwa zinaingia moja kwa moja kwenye michuano mikubwa ya Afrika- Kombe la Washindi, Kombe la CAF na Klabu Bingwa Afrika.
  Julai na Agosti ni kipindi ambacho michuano ya CAF inafikia kwenye hatua ya makundi- lakini kwa sababu Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limejikatia tamaa, halioni umuhimu tena wa michuano hiyo ya bara zima.
  Sasa ni dhahiri sisi wa CECAFA ndiyo tunashika mkia kisoka katika bara letu, hata nchi ndogo ndogo zilizokuwa duni kisoka miaka michache iliyopita kama Madagascar, Lesotho, Swaziland na Shelisheli za kusini (COSAFA) sasa zinatufundisha mengi. 
  Hii ni kwa sababu, pamoja na mapungufu yetu yote, lakini pia hatuna mipango.
  Mfano mdogo ni hii michuano ya Kagame, badala ya kuifanya Januari ili timu zetu zipate maandalizi ya kuingia kwenye michuano ya Afrika, tunaifanya Julai na Agosti.
  Mashindano hayo yakirudi kufanyika Januari, dhahiri yatarejesha msisimko wake na hakutakuwa na udhuru wa timu kutokuja kushiriki.
  Hata ile dhamira ya kualika timu kubwa za ukanda mwingine kuja kutongezea changamoto inaweza kufanikiwa kwa sababu hicho ni kipindi ambacho hakuna mashindano ya CAF.
  Lazima turejeshe enzi zile bingwa mtetezi anapokewa kwenye kituo cha mashindano akiwa na Kombe lake. Turejeshe enzi ambazo mashindano yanashirikisha mabingwa watupu wa ukanda wetu.
  Turejeshe thamani ya mashindano kwamba si ya kila timu kushiriki, yawe mashindano ya mabingwa wa ukanda wetu.
  Novemba na Desemba tunafanya Challenge (Kombe la Mataifa ya CECAFA), Januari mapema tu ndani ya wiki mbili za mwanzo tunakamilisha Kagame- baada ya hapo, klabu zetu ziende kwenye michuano ya Afrika zikiwa vizuri.
  Lakini ajabu CECAFA wameshindwa kuelewa dhana hii na wameendelea kulazimisha Kombe la Kagame lifanyike Agosti, ndiyo maana watu sasa wanayaita mashindano haya Bonanza tu, kwa sababu hawaoni umuhimu wake.
  Katika miaka yote 10 ya Leodegar Chillah Tenga wa Tanzania kuwa Rais wa CECAFA ameshindwa kuupokea ushauri wa kuirudisha Januari michuano ya Kagame, lakini baada ya Novemba mwaka jana kupatikana Rais mpya, Mutasim Sirelkhatim Gaffar wa Sudan, tunasubiri naye tumuone atachukua gani kuinusuru soka ya ukanda huu. Au naye haambiliki?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: RAIS MPYA CECAFA NAYE ‘HAAMBILIKI’? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top