• HABARI MPYA

    Wednesday, January 20, 2016

    KIKWAZO CHA MABADILIKO SIMBA NA YANGA NI VIONGOZI WAKE WENYEWE

    MIAKA ya 1990 idadi kubwa ya wanachama waliokuwa wakihudhuria 
    mikutano ya klabu kongwe nchini, Simba na Yanga haikuzidi 300.
    Na ni wakati huo, ambao wanachama wengi walikuwa hawalipii ada za uanachama wao, hadi unapowadia wakati wa uchaguzi na iliaminika wengi walikuwa wanalipiwa na wagombea.
    Mwanzoni mwa miaka ya 2000, taratibu idadi ikaanza kuongezeka na hadi kufika sasa Mkutano mmoja wa klabu moja unaweza kuhudhuriwa na zaidi ya wanachama 1000, lakini hawafiki 2000.

    Ingawa ukienda kwenye vitabu vya orodha za wanachama, kila klabu ina wanachama zaidi ya 10,000 kwa sasa.
    Na hao ndiyo unaweza kusema ndiyo wamiliki wa klabu hizo – wengi wao wakiwa ni vijana wa kizazi cha sasa wenye umri kati ya miaka 18 hadi 30.
    Simba na Yanga zilikuwa zina wafuasi wengi tangu miaka ya 1940, lakini ni siku za karibuni zimeanza kuwa na wanachama wengi.
    Ongezeko hilo limetoana na kampeni za kuhamasisha wapenzi kuwa wanachama kwa kununua kadi.
    Siku hizi, kadi za uanachama wa Simba na Yanga zinapatikana holela tu. Mtu analipia, anapewa tofauti na miaka ya nyuma kulikuwa kuna urasimu wa hali ya juu. Zamani mtu kuwa na kadi ya uanachama wa Simba, au Yanga ilikuwa daraja fulani.
    Kulikuwa kuna watu wenye uwezo wa kifedha na watumishi wakubwa wa umma waliokuwa na mapenzi na timu hizo, lakini walisotea kadi za uanachama.
    Kupatikana holela kwa kadi za uanachama za klabu hizo rasmi kumeanza miaka ya 2000.
    Vyema, sasa klabu hizo zimekuwa za wengi ingawa kwa sababu hiyo pia zimeanza taratibu kuondokana na miiko na taratibu zake za asili.
    Sitaki kwenda mbali sana katika kujadili asili na historia ya klabu hizo – maana ni ndefu, tena ndefu sana.
    Jambo moja tu la kusikitisha ni kwamba ongezeko la idadi ya wanachama haliendani na ongezeko la thamani au rasilimali za klabu hizo. 
    Rasilimali kubwa za Simba ni majengo yake mawili pacha yaliyopo Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam. Jengo la kwanza la Simba lilijengwa kwa mchango wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amaan Karume na wanachama wa klabu hiyo wakaongezea fedha na wakashiriki ujenzi, wakibeba, zege, mchanga, kokoto- yaani vifaa vya ujenzi kwa ujumla na hata kufyatua tofali. Jengo kuu la Simba lilijengwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti Rahim Dumelezi  na Katibu Mkuu Said Mpolaki (wote sasa marehemu).
    Jengo la pili lilijengwa kwa mpango maalumu wa mkataba na mtu aliyeamua kuwekeza kwenye kiwanja cha wazi cha klabu hiyo. Mwekezaji aliruhusiwa kujenga na kutumia jengo kwa biashara zake hadi mwaka 2012 alikabidhi kwa klabu.
    Mpango kamili wa ujenzi wa jengo hilo ulioanzishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Simba, Kassim Mohamed Dewji, ni kuwa na ghorofa nane katika mtindo huo wa makubaliano na watu wenye nia ya kuwekeza kwenye jengo hilo.
    Mwekezaji huyo angeweza kuendelea na ujenzi wa jengo hilo, kama wanachama wa klabu hiyo wasingefungua kesi mahakamani kupinga zoezi hilo. Limeishia kwenye ghorofa mbili, ambazo pia ujenzi wake haujakamilika ipasavyo.
    Simba SC zaidi ya hapo haina japo Uwanja wa mazoezi, ingawa ina eneo Bunju ambako wamekuwa na mpango usiotimia wa kujenga Uwanja wa kisasa.
    Baada ya porojo za ujenzi wa Uwanja wa kisasa kuzoeleka, sasa hadithi mpya ni mwanachama na mfadhili wa klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe kutaka kuijengea klabu Uwanja wa mazoezi. Tumpe muda na tumuombee afya na uzima atekeleze ahadi yake.   
    Kwa upane wa Yanga ni majengo yao mawili, dogo la Mtaa wa Mafia na kubwa la Jangwani lilio sambamba na Uwanja wa Kaunda. Baada ya kuwa chakavu kwa muda mrefu, jengo hilo lililojengwa kwa msaada wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Abeid Karume aliyechangia Sh milioni 2.7 kwa ajili ya ujenzi, hivi karibunu lilikarabatiwa na mfadhili wao, Yussuf Mehboob Manji ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu.
    Jengo la Yanga halijawahi kuwa katika mwonekano mzuri kama huu wa sasa, lina klabu ya mazoezi ya viungo (gym) ya kisasa, bwawa la kuogelea, ukumbi wa mikutano, ofisi na eneo la kuegesha magari.
    Manji aliibuka Yanga mwaka 2006 na kuingia mkataba wa kuifadhili klabu hiyo, chini uongozi wa Francis Mponjoli Kifukwe na kwa kipindi kifupi, ameibadilisha klabu hiyo angalau sasa inaonekana.
    Hata hivyo, siku za karibuni mandhari ya jengo imeanza kuharibika tena kutokana na kukosa matunzo.
    Pia wana Uwanja wa Kaunda uliojengwa kwa mkopo wa Sh 500,000 wa Benki ya Nyumba (THB) ambao awali ulikuwa unavutia watu wengi wakati wa mazoezi ya timu hiyo.
    Kwa sasa Uwanja wa Kaunda hautumiki tena kutokana na kutelekezwa – na kumekuwa na hadithi za muda mrefu za ujenzi wa Uwanja wa kisasa zisizotimia.
    Kikubwa ni kwamba, miaka inakatika na mambo mengi yanabadilika Dar es Salaam, lakini sura za Simba na Yanga ni zile zile na hakuna dalili za mabadiliko.
    Ukiuliza kikwazo kikubwa utaambiwa ni wanachama – wakati ukizama ndani haswa unagundua tatizo ni viongozi wenyewe wanaopewa dhamana ya kuongoza klabu hizo kutokuwa tayari kwa mabadiliko.
    Ukweli ni kwamba idadi kubwa ya wapenzi na wanachama wa kisasa wa klabu hizo wanataka sana mabadiliko, tatizo viongozi wenyewe hawako tayari kwa hilo.
    Nini kifanyike kushinikiza mabadiliko ndani ya klabu hizo? Tukijaaliwa Jumapili nitaendelea. Asanteni. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIKWAZO CHA MABADILIKO SIMBA NA YANGA NI VIONGOZI WAKE WENYEWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top