• HABARI MPYA

    Sunday, January 31, 2016

    YONDAN AWAOMBA RADHI YANGA KWA KADI NYEKUNDU NA KIPIGO CHA COSTAL, ASEMA WANAJIPANGA UPYA WASIRUDIE MAKOSA

    Na Salma Isihaka, TANGA
    BEKI wa Yanga SC, Kevin Yondan (pichani kulia) amewaomba radhi mashabiki wa timu hiyo baada ya jana kutolewa kwa kadi nyekundu, timu yake ikilala 2-0 mbele ya Coastal Union.
    Yanga SC ilipoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, baada ya kufungwa mabao 2-0 na wenyeji Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
    Na refa Andrew Shamba alimtoa kwa kadi nyekundu Yondan dakika ya 100 akitoka kujichanganya kwa kumuonyesha kadi nyekundu Said Jeilan wa Coastal badala ya njano dakika ya 97.
    “Ni mambo ambayo yanatokea kwenye soka, kikubwa napenda niwaombe radhi mashabiki wa timu yangu, Yanga kwa kuonyeshwa kadi nyekundu. Na nitajitahidi hali kama hii isijitokeze tena,”amesema.
    Aidha, Yondan amewaomba radhi mashabiki wa Yanga kwa matokeo ya jana, akisema ni hali ya mchezo ambayo hata wao wachezaji hawakuifurahia.
    “Naweza kusema kama mchezo ulitukataa, maana tulicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi tu ila tukashindwa kutumia, lakini wenzetu wakatumia nafasi zao mbili tu walizopata, wakashinda mechi. Haikuwa bahati yetu,”amesema.
    Yondan amesema wanakwenda kujiuliza kama timu kwa maana ya benchi la ufundi na wachezaji ili warekebishe makosa yao na kuhakikisha wanarejesha wimbi la ushindi katika Ligi Kuu.   
    Yanga SC sasa wanatarajiwa kusafiri kwenda mjini Mbeya kwa ajili ya mchezo dhidi ya Prisons Jumatano Uwanja wa Sokoine.
    Kipigo cha jana kimeiyumbisha kidogo Yanga SC katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, sasa ikiwa imecheza mechi 16 na kuvuna pointi 39, wakati Azam FC iliyocheza mechi 15 ina pointi 39 pia na mahasimu wao, Simba SC waliocheza mechi 16, wana pointi 36.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YONDAN AWAOMBA RADHI YANGA KWA KADI NYEKUNDU NA KIPIGO CHA COSTAL, ASEMA WANAJIPANGA UPYA WASIRUDIE MAKOSA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top