• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 27, 2016

  HII KALI, AZAM FC WANAACHA LIGI WANAKWENDA KWENYE BONANZA!

  NAJARIBU kujiuliza, iko siku Ratiba ya Ligi Kuu ya Zambia itafanyiwa marekebisho madogo ili kuipa fursa moja ya timu za ligi hiyo kwenda kushiriki michuano ya kirafiki nje?
  Sidhani. Nasema sidhani kwa sababu moja ya ligi bora hapa barani, ni ya Zambia maarufu kama MTN/FAZ Super Division, inayoendeshwa kwa nidhamu ya hali ya juu na kuzingatia taratibu walizojiwekea.
  Lakini imetokea Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imefanyiwa marekebisho madogo, ili klabu ya hapa, Azam FC iende Zambia kucheza michuano ya kirafiki.
  Azam FC iliondoka usiku wa juzi kwenda Zambia kushiriki michuano maalum na inatarajiwa kurejea Februari 4, mwaka huu.

  Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alikaririwa akisema kwamba wamepata ruhusa maalum kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya ziara yao na mechi zao hizo mbili za Ligi Kuu zitapangiwa tarehe nyingine.
  Mechi hizo ni dhidi ya Prisons iliyokuwa ifanyike Uwanja wa Sokoine, Mbeya Jumamosi wiki hii na dhidi ya Stand United iliyopangwa kufanyika Februari 3, mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Kawemba amesema kwamba watakaporejea Februari 4, wataendelea na ratiba watakayoikuta ya Ligi Kuu, kuanzia mchezo na Mwadui FC Februari 7, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
  Na Kawemba alisema mechi zao za viporo zitachomekwa katikati ya ratiba yao kuanzia hapo kulingana na nafasi ambayo itaonekana inafaa kwao na kwa wapinzani wao.
  Azam FC imealikwa nchini Zambia kushiriki michuano maalumu inayoshirikisha timu nne, iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa klabu mbili za huko, Zesco United na Zanaco FC.
  Michuano hiyo inaanza leo Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola na mbali na Azam FC, Zesco na Zanaco, timu nyingine itakayoshirki mabingwa wa Ligi Kuu Zimbabwe, Chicken Inn.
  Mara baada ya Azam FC kusafiri, wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Yanga SC nao wakasema watakwenda Afrika Kusini Ijumaa kuweka kambi ya kujiandaa na mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrima mapema mwezi ujao. Yanga SC inataka kuondoka nchini siku moja kabla ya mchezo wake wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union ya Tanga uliopangwa kufanyika Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro alikaririwa akisema kwamba kikosi cha Yanga kitatumia fursa hiyo kama sehemu ya maandalizi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza mwezi ujao.
  Muro amesema Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Deusdedit Baraka atawasilisha barua TFF kuomba kusogezwa kwa michezo yao kadhaa ili waweze kwenda Afrika Kusini.
  Azam FC imeruhusiwa, lakini Yanga SC hawajaruhusiwa – maana yake ratiba ya mechi nyingine za Ligi Kuu inabaki kama ilivyo na itaendelea Jumamosi, Coastal Union wakiikaribisha Yanga SC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Simba SC wakiwa wenyeji wa African Sports wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mechi nyingine ni kati ya JKT Ruvu na Majimaji Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Mtibwa Sugar na Stand United Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Mwadui FC na Toto Africans Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na Kagera Sugar dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Mwinyi, Tabora. 
  Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja tu, kati ya Mgambo JKT na Ndanda FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Makosa yamefanyika kuiruhusu Azam FC kwenda ziarani Zambia katikati ya Ligi Kuu.
  Itafikiriwa Azam FC kwamba itajibebesha mzigo wa kucheza mechi mbili katika nafasi ya mechi moja, na kwa kuwa wametaka wao wenyewe si vibaya, - lakini vipi hao wapinzani wao walioahirishiwa mechi?
  Namaanisha Prisons na Stand United ambao itabidi nao wacheze mechi mbili katika nafasi ya mechi moja, bila makosa yoyote.
  Kwa mara nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linaainisha mapungufu yake katika uendeshaji wa mchezo huo nchini katika suala hili.
  Jamal Malinzi, Rais wa TFF anajifikiriaje katika suala hili- Ligi Kuu imekuwa ya mzaha, achilia mbali kanuni mbovu zilizosababisha mlundikano wa wachezaji wa kigeni, sasa imekuwa pia ligi ambayo haina adabu.
  Ligi kama gari bovu inaweza kusimama wakati wowote bila sababu yoyote ya msingi. Hii ni hatari. 
  Naomba iwe Yanga wanatania tu na wasiende huko Afrika Kusini, ili Ligi Kuu isiingie dosari zaidi, lakini wakiamua kukomaa kweli, watazuiwa vipi ikiwa wapinzani wao wamepewa fursa hiyo?
  Na timu nyingine yoyote ya Ligi Kuu ikiwasilisha mwaliko wake TFF, inawezaje kuzuiwa ikiwa tayari Azam FC wameruhusiwa? Kuna tatizo. Kawemba amekaa pale TFF katika kitengo cha nyeti sana wakati wa Rais Leodegar Tenga, nadhani anajua Azam FC wameruhusiwa kimakosa.
  Na Azam FC wametumia mwanya wa udhaifu wa TFF kufanikisha yao – ingawa ziara hiyo hata wao haitawasaidia na zaidi inaweza kuwaathiri tu.
  Azam FC watacheza mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Machi 11 dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini –ndiyo leo wanakwenda Zambia kujiandaa kwa mchezo huo?
  Haiingii akili hata kidogo na ninachokiona wachezaji wanakwenda kuchoshwa tu na kujipotezea kile kinaitwa ‘timing’ katika mawindo yao ya ubingwa wa Ligi Kuu.
  Na sitaki kuamini kama benchi la Ufundi makini chini ya makocha wataalamu wakiongozwa na Muingereza Stewart Hall linaweza kukubali kitu kama hicho.
  Hoja ya muda wa kutosha wa maandalizi kabla ya mechi za michuano ya Afrika ni muhimu kwa wawakilishi wote, Azam na Yanga lakini pia lazima dhana ibebe maana halisi.
  Tunaiondoa timu katika Ligi Kuu takriban siku 50 kabla ya mechi ya CAF, eti inapewa fursa ya maandalizi, huu ni mzaha wa hali ya juu.
  Makosa yamekwishafanyika na Azam FC tayari ipo Ndola ambako leo itacheza mchezo wa kwanza – lakini si vyema tukairuhusu Ligi yetu kuwa ya kuchezewa namna hii.
  Na kwa Azam FC pia, bodi ya Ukurugenzi wakati mwingine itafakari mawazo au mapendekezo ya watu iliyowapa dhamana ya kuongoza timu yao – maana ninachokiona hapa ni kuwachosha wachezaji.
  Wanakwenda kucheza mechi tatu ndani ya wiki moja na wakirudi katika Ratiba ya Ligi Kuu watalazimika kucheza mechi nne ndani ya wiki moja – ikiwa itakuwa kama alivyosema Kawemba kwamba watacheza mechi mbili katika nafasi ya mechi moja, ili kufidia na viporo vyao.
  Nasubiri kuona Azam FC itamudu vipi kucheza mechi mbili katika nafasi ya mechi moja, tena katika wakati ambao ipo kwenye mbio za ubingwa.
  Yanga hawatakwenda Afrika Kusini ninaamini. Watakwenda kuvuna pointi Tanga na watarejea kwenye ratiba yao mechi nyingine kabla ya kusafiri kwenda Mauritius kumenyana na Cercle de Joachim katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika Februari 13.  
  Naanza kuona dalili za Azam FC kuukosa tena ubingwa wa Ligi Kuu tu kwa sababu ya mapungufu ya uongozi wao wenyewe. Ni juu yao, lakini TFF inazidi kuanisha udhaifu wake kwa kuwaruhusu Azam FC kuacha Ligi waende kwenye mechi za kirafiki ‘bonanza’ Zambia. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HII KALI, AZAM FC WANAACHA LIGI WANAKWENDA KWENYE BONANZA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top