• HABARI MPYA

  Jumapili, Januari 24, 2016

  NAPE ANAWEZA KUSAIDIA MABADILIKO SIMBA NA YANGA IWAPO...

  KAMA nilivyoahidi Jumatano, leo najaribu kujadili suluhisho la matatizo ya klabu kongwe nchini, Simba na Yanga SC.
  Katika makala yangu ya Jumatano nilizungumzia namna ambavyo viongozi wa klabu hizo wameshindwa kufanikisha dhana ya mabadiliko – huku wanachama wakisingiziwa kuwa kukwazo.
  Naikataa dhana ya kwamba wanachama wa Simba na Yanga ndiyo kikwazo cha mabadiliko kutokana na ukweli kwamba zama zimebadilika mno.
  Asilimia kubwa ya wanachama na wapenzi wa sasa wa klabu hizo ni watu wenye uelewa na mitazamo ya kisasa, tofauti na wale wa miaka ya nyuma ambao kweli walikuwa kikwazo.
  Hivi karibuni, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro alipotoka akasema maneno yaliyochukuliwa kama ya kibaguzi, akijinasibu yeye ni Mchaga aliyekuja mjini kutafuta fedha na si Mzaramo ‘mpiga umbea’ mjini.
  Watu walitaka kumsakama Muro na kwa sababu alisema maneno hayo dhidi ya Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa wapinzani, Simba SC – Hajji Manara mambo yakataka kukuzwa.
  Lakini tunashukuru yameisha. Ukweli ni kwamba Muro alizungumzia asili na mazoea ya watu wa asili wa Dar es Salaam, wengi wao walikuwa hawapendi kufanya kazi kujitafutia maendeleo.
  Walikuwa wanapenda kukaa kwenye vijiwe na mabaraza ya mazungumzo wakicheza michezo ya kivivu kama bao, drafti, karata, dhumna na kadhalika.
  Lakini hao si watu wa Dar es Salaam ya sasa – mambo yamebadilika na sasa karibu kila Mtanzania anapenda kufanya kazi kujitafutia maendeleo na hiyo ndiyo siri ya kupotea kwa umaarufu wa michezo ya kivivu jamii ya bao na karata.
  Kwa ujumla Watanzania wa leo wanapenda maendeleo yao binafsi, maendeleo ya jamii zao na hata matabaka yao, yawe ya kimila, desturi au dini.
  Vivyo hivyo na hata kwa wapenzi wa klabu za Simba na Yanga sasa wanatamani maendeleo zaidi kwa klabu zao, ili ziendane na klabu nyingine kubwa barani mfano TP Mazembe ya DRC, ambayo imekuwa kigezo kizuri kwao tangu iwe na wachezaji wa Kitanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
  Lakini wanabaki kuendelea kuzipenda timu zao kwa sababu hawana namna nyingine, japo zinawakera kutokana na kutobadilika ziendane na aina ya klabu kama TP Mazembe.
  Nini tunaamini kitafanyika kushinikiza mabadiliko ndani ya klabu hizo, ikiwa safu za uongozi zimekuwa zikibadilika lakini taswira ya klabu inabaki vile vile miaka nenda, miaka rudi?
  Serikali. Ndiyo, Serikali ndiyo jibu la suluhisho la matatizo ya Simba na Yanga.
  Wote tunaamini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sasa chini ya Rais wake, Jamal Malinzi lina ushirikiano mzuri na Serikali na hakuna misigano.
  TFF inapenda kuona Simba na Yanga zinakuwa klabu kubwa kwa maana halisi, ili ziweze kuchangia vyema maendeleo ya soka ya nchi hii.
  TFF inapenda kuona Simba na Yanga zinakuwa na misingi mizuri ya kuibua, kuzalisha na kuendeleza vipaji, ili baadaye vije kulisaidia taifa katika medani ya kimataifa.
  TFF inapenda kuona Simba na Yanga zinakuwa vizuri kiuchumi ili ziweze kushiriki vyema na kwa mafanikio kwenye michuano mikubwa ya Afrika.
  TFF inapenda kuona Simba na Yanga zinakuwa daraja zuri la wachezaji wa Tanzania kwenda kucheza Ulaya, ili wakapate ujuzi na uzoefu zaidi baadaye waje kuzisaidia timu zetu za taifa kuanzia za vijana.
  TFF inatamani kila zuri juu ya klabu hizo kongwe zenye wapenzi wengi, ikiamini huo ndiyo utakuwa mwanzo mpya wa ustawi wa soka ya nchi hii.
  Lakini haina uwezo wa kuziingilia kinyume cha mamlaka iliyonayo, labda kuzishauri tu – jambo ambalo limekuwa likifanya na vyombo vya habari kwa muda bila mafanikio.
  Lakini Serikali inaweza, hususan hii ya awamu ya tano ya Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli ya ‘Kazi kazi tu’. Inaweza.
  Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, chini ya Waziri wake Nape Nnauye ina wajibu wa kusimamia michezo nchini kikamilifu ili kufanikisha ustawi wake.
  Nape na timu yake pale Wizarani, wanapaswa kuja na maarifa na mikakati mipya katika kwanza kuliinua gurumu la maendeleo ya soka nchini, ambalo lina pancha kwa sasa, kabla ya kuanza kulisukuma mbele.
  Nape anahitaji kuweka mpango mkakati mzuri wa kuleta mabadiliko katika sekta ya michezo Tanzania, badala ya kubaki tu kuwa mtu wa kualikwa alikwa awe mgeni rasmi kwenye shughuli za michezo.
  Nape anahitaji kuzama ndani katika kutafuta tiba halisi ya maradhi ya michezo nchini – badala ya kubaki kuwa Waziri wa kupongeza mafanikio yanayokuja kwa ngekewa.
  Soka ukiwa mchezo mkubwa zaidi na Simba na Yanga SC zikiwa klabu kubwa zaidi, ni sehemu nzuri kwake Nape na timu yake kuanzia katika kujaribu kuleta mabadiliko.
  Inawezekana. Hakuna aliye mkubwa kuliko Serikali na kama suala ni kuzifanya klabu hizo ziwe kubwa kiuchumi na zenye muundo wa kisasa utakaotengeneza mazingira ya kuzifanya zifanikiwe ndani na nje ya Uwanja, nani atapinga?
  Ninaamini, wakati sasa umefika Serikali mpya ya awamu ya Tano ikavalia njuga matatizo sugu ndani ya klabu za Simba na Yanga ili kusaidia kuleta mabadiliko.
  Nchi hii ina wataalamu wa kutosha wa masuala ya michezo kwa sasa na wasomi ambao wanaweza kutoa mwongozo mzuri wa nini kifanyike, Simba na Yanga siku moja zizungumziwe kama klabu kubwa barani.
  Na kama hatuwaamini wataalamu wetu, basi tutumie wataalamu wa nje, ambao kwa kushirikiana na Wizara ya Nape – ninaamini wanaweza kutufanya ndani ya muda mfupi tusizisahau Simba na Yanga za kizamani. Alamsiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NAPE ANAWEZA KUSAIDIA MABADILIKO SIMBA NA YANGA IWAPO... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top