• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 27, 2016

  YANGA SC WAAMUA ‘KUIPOTEZEA’ AFRIKA KUSINI, WANAONDOKA KESHO DAR KUFUATA POINTI TATU KWA COASTAL UNION

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imefuta mpango wa kwenda Afrika Kusini Ijumaa na sasa itasafiri kesho kwenda Tanga kwa ajili ya mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani.
  Yanga SC ilitaka kwenda Afrika Kusini kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wake wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim Februari 13, mwaka huu nchini Mauritius.
  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu kwamba kikosi cha Yanga kitaondoka kesho kwenda Tanga kwa ajili ya mechi na Coastal.
  Badala yake, Yanga SC wako katika mpango wa kuialika timu moja ya nje ije kucheza nao mchezo wa kirafiki, kabla ya kwenda Mauritius.
  Yanga SC wanakwenda Tanga kesho kuifuata Coastal Union

  Yanga SC walitangaza ziara ya Afrika Kusini juzi, baada ya wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Azam FC kuahirishiwa mechi mbili za Ligi Kuu, dhidi ya Prisons uliokuwa ufanyike Uwanja wa Sokoine, Mbeya Jumamosi wiki hii na dhidi ya Stand United uliopangwa kufanyika Februari 3, mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kufutwa ili waende Zambia.
  Azam FC ipo Zambia tangu juzi kushiriki michuano maalum na leo imetoa sare ya 1-1 na Zesco United katika mchezo wa kwanza – na inatarajiwa kurejea Februari 4, mwaka huu.
  Azam FC imealikwa nchini Zambia kushiriki michuano maalumu inayoshirikisha timu nne, iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa klabu mbili za huko, Zesco United na Zanaco FC. Timu nyingine itakayoshirki mabingwa wa Ligi Kuu Zimbabwe, Chicken Inn.
  Pamoja na Azam FC kuruhusiwa kwenda Zambia, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea Jumamosi, Coastal Union wakiikaribisha Yanga SC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Simba SC wakiwa wenyeji wa African Sports wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mechi nyingine ni kati ya JKT Ruvu na Majimaji Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Mtibwa Sugar na Stand United Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Mwadui FC na Toto Africans Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na Kagera Sugar dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Mwinyi, Tabora. 
  Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja tu, kati ya Mgambo JKT na Ndanda FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WAAMUA ‘KUIPOTEZEA’ AFRIKA KUSINI, WANAONDOKA KESHO DAR KUFUATA POINTI TATU KWA COASTAL UNION Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top