• HABARI MPYA

  Jumamosi, Januari 30, 2016

  HANS POPPE AWAKUMBUSHIA TP MAZEMBE 'MAHELA' YA SIMBA SC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba wanasubiri mgawo wao wa Euro 160,000 kutoka klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutokana na mauzo ya mshambuliaji Mbwana Ally Samatta.
  Samatta alijiunga na Mazembe mwaka 2011 kwa dau la Sh. Milioni 100,000 akitokea Simba SC na jana ametambulishwa rasmi kujiunga na klabu ya Koninklijke Racing Club Genk kwa Mkataba wa miaka minne na nusu.
  “Kwa sasa tunasubiri mgawo wetu tu kutoka Mazembe, ambao ni asilimia 20 ya mauzo ya Samatta kwenda Genk,”amesema Hans Poppe aliyefanikisha usajili wa Samatta mwaka 2010 kutoka African Lyon. 
  Hans Poppe amesema wanasubiri mgawo wa mauzo ya Samatta kutoka TP Mazembe

  BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu Samatta ameuzwa kwa Euro 800,000 Genk kutoka Mazembe ambayo italazimika kuipa Simba SC asilimia 20 ya pato hilo kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
  Na Nahodha huyo wa Tanzania ameishukuru Mazembe kwa kumchukua akiwa kijana mdogo na kumlea vizuri na kukuza kipaji chake hadi kutimiza ndoto ya kucheza Ulaya.
  KRC Genk imetimiza ndoto za kumpata mshambuliaji bora, Samatta aliyewasili juzi Brussels na moja kwa moja kusafiri hadi Genk kutambulishwa.
  Samatta aliyezaliwa Desemba 23, mwaka 1992, anaondoka Mazembe baada ya kushinda nayo taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, ubingwa wa Ligi Kuu ya DRC mara nne na Super Cup ya DRC mara mbili.
  Ukiacha Euro 160,000, Simba SC pia inatarajia kulipwa dola za Kimarekani 300,000 za mauzo ya mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka 2013.
  Samatta alitokea Simba SC kwenda TP Mazembe kabla ya kuuzwa KRC Genk

  Etoile wamekuwa wazito kulipa fedha hizo kwa sababu walidumu na Okwi kwa miezi sita kabla ya kushindwana na kushitakiana hadi FIFA.
  Etoile ilimtuhumu Okwi kuchelewa kurejea klabuni baada ya kuruhusiwa kwenda kuchezea timu yake ya taifa, wakati mchezaji akadai kutolipwa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu. 
  Mwishowe Okwi aliruhusiwa na FIFA kutafuta klabu ya kuchezea wakati kesi yake na Etoile inaendelea – naye akarejea klabu yake ya zamani, SC Villa ya Uganda, ambayo baadaye ilimuuza Yanga SC mwaka 2014.
  Baada ya nusu msimu, Okwi akavurugana pia na Yanga hadi kufikishana TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) ambako aliruhusiwa kuondoka bure Jangwani, hivyo kujiunga tena na Simba SC kama mchezaji huru.
  Simba SC ikamuuza tena Okwi kwa dola za Kimarekani 100,000 klabu ya SonderjyskE ya Ligi Kuu ya Denmark, ambako anakoendelea na kazi hadi sasa. 
  Desemba mwaka jana, FIFA iliipa Etoile siku 60 kuwa imekwishalipa dola 300,000 za Simba SC, vinginevyo watachukuliwa hatua kali, ikiwemo kufungiwa kucheza mashindano yoyote. 
  Mbwana Samatta (kushoto) ndiye Nahodha wa Tanzania kwa sasa akiwa ana umri wa miaka 24 tu
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HANS POPPE AWAKUMBUSHIA TP MAZEMBE 'MAHELA' YA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top