• HABARI MPYA

  Jumamosi, Januari 23, 2016

  CHANJI AJIBU TUHUMA ZA KUMNG’OA DK TIBOROHA YANGA, ASEMA; “JAMAA ALIVYOVURUNDA MUNGU ANAJUA”

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Isaac Chanji amesema hana tatizo na aliyekuwa na Katibu Mkuu wa klabu, Dk Jonas Tiboroha, bali utendaji wake usioridhisha ndiyo umemuondoa kazini.
  Aidha, Chanji amesema kwamba Tiboroha ameondoka Yanga SC kutokana na tuhuma mbalimbali zilizokuwa zinamkabili mbele ya Kamati ya Utendaji, ikiwemo utendaji usioridhisha na kupoteza uaminifu.
  “Si kweli,”amesema Chanji akikana madai kwamba amesababisha Tiboroha kuondoka Yanga SC.
  “Huyu bwana awaambie watu ukweli, kwamba alipewa fursa ya kujiuzulu mwenyewe kulinda heshima yake, baada ya kubainika dosari nyingi katika utendaji wake,”amesema Chanji.
  Isaac Chanji (kushoto) amesema hahusiki na kujiuzulu kwa Dk Tiboroha

  Miongoni mwa tuhuma ambazo zimemtoa Tiboroha Yanga SC ni pamoja na kuajiri watu bila ridhaa ya Kamati ya Utendaji, kusafiri kwenda Ghana kwenye kongamano la Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) bila ridhaa ya mwajiri wake, huku akiaga ameenda kwao Kigoma kwa matatizo ya kifamilia.
  Mapema leo, Tiboroha ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE kwamba amejiuzulu ili apate muda zaidi wa kufanya shughuli zake za Uhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
  Dk. Jonas Tiboroha (wa pili kulia) sasa si Katibu wa Yanga tena

  “Mimi ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitivo cha Elimu ya Viungo (PE), na kwa kuondoka Yanga SC maana yake napata wasaa mzuri wa kumtumikia mwajiri wangu, UDSM,”amesema.
  Tiboroha aliingia Yanga SC Desemba mwaka 2014 akichukua nafasi ya Benno Njovu aliyeondolewa kwa tuhuma mbalimbali. Aliingia Yanga SC akitokea Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama Ofisa Maendelezo ya Ufundi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHANJI AJIBU TUHUMA ZA KUMNG’OA DK TIBOROHA YANGA, ASEMA; “JAMAA ALIVYOVURUNDA MUNGU ANAJUA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top