• HABARI MPYA

  Jumatatu, Januari 25, 2016

  CHEKA AREJEA NCHINI KWA MAANDALIZI YA MWISHO PAMBANO LAKE NA MUINGEREZA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BONDIA maarufu wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka amerejea nchini kutoka Zambia na kusema Mserbia Geard Ajetovic aiandae kupokea kipigo kikali katika pambano lao la kuwania wa Mabara wa WBF, uzito wa Super Middle.
  Cheka na Ajetovic watapambana kwenye viwanja vya Leaders Club Februari 27 katika pambano
  lililoandaliwa na kampuni ya Hall of Fame Boxing & Promotion.
  Akizungumza leo mjini Dar es Salaam, Cheka alimpongeza  meneja wake, Juma Ndambile wa Kampuni ya Advanced Security Limited kwa kumwezesha kuweka kambi nje ya nchi ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya mchezo huo kwa upande wake.
  Francis Cheka (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wake, Juma Ndabila

  Alisema kuwa Ndambile na kampuni yake imeonyesha kuwa wanajali na wanamalengo makubwa ya
  kumwendeleza kutokana na ukweli kuwa amekaa katika kambi ya kisasa yenye
  mabondia na makocha wazuri nchini Zambia.
  “Kwanza naishukuru kampuni ya Advanced Security Limited kwa kufanikisha kambi hii, nimejifua vya kutosha nchini Zambia, mazoezi yalikuwa magumu na yalihitaji uvumilivu mkubwa, kwa kutambua lengo langu ni nini, nilifanya kwa juhudi zote na sasa nipo tayari kwa pambano, hata kesho (leo) nipo tayari kwa bondia yoyote duniani,” alisema Cheka.
  Alisema kuwa kutokana na siku kuwa nyingi, ataendelea na mazoezi hapa hapa nchini huku akisubiri mipango mengine ya meneja wake kwa upande wa maandalizi.
  Meneja wa Cheka, Juma Ndambile ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Advanced Security Limited alisema kuwa  lengo la kampuni yao ni kufanya mapinduzi na kuleta maendeleo katika mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini.
  Ndambile alisema kuwa Cheka ni bondia mwenye kipaji na hakuwa tayari kuona kipaji hicho kinapotea na kuchukua jukumu la kumwendeleza. “Mimi na kampuni yangu tuna mipango ya kuwamiliki mabondia wengi hapa nchini, kama ilivyo kwa Cheka, nao watapata fursa ya kufanya mazoezi nje ya nchi na kupata mapambano ya kimataifa ya ubingwa ili kuiletea sifa taifa,” alisema Ndambile.
  Alisema kuwa wanataka kutumia vizuri fursa waliyopewa na WBF ambayo inamtaka Cheka ashinde pambano hilo ili aweze kuwania ubingwa wa Dunia hapa hapa nchini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHEKA AREJEA NCHINI KWA MAANDALIZI YA MWISHO PAMBANO LAKE NA MUINGEREZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top