• HABARI MPYA

    Sunday, June 14, 2015

    HIVI WATU WANAFIKIRI WATANZANIA NI WAJINGA KIASI GANI?

    MIGUNO ilitawala ndani ya ukumbi wa JB Belmonte (Kilimanjaro) uliopo katika jengo la Golden Jubilee Tower (PSPF), mtaa wa Ohio, Dar es Salaam, wakati wa utoaji wa tuzo za washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Ni tuzo mbili tu, ambazo zote alichukua Simon Happygod Msuva ambazo watu hawakuguna- lakini nyingine zote waalikwa mbalimbali wakiwemo Waandishi wa Habari waliguna.
    Mshambuliaji, Simon Msuva alibeba tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu akiwashinda beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba SC na Mrisho Ngassa waliyekuwa naye Yanga SC kabla ya kutimkia Afrika Kusini.
    Kwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu, alipata jumla ya Sh. Milioni 11.4, yaani Sh. Milioni 5.7 kwa kila tuzo aliyotwaa usiku wa leo. 
    Shaaban Kado aliyetupiwa virago Coastal Union mwishoni mwa msimu alishinda tuzo ya kipa bora wa msimu na kuwabwaga wenzake Mohamed Yusuph wa Tanzania Prisons na Said Mohamed wa Mtibwa Sugar kutwaa tuzo hiyo ya kipa bora na kujinyakulia Sh. Milioni 5.7.
    Kipa wa zamani wa Yanga SC, Mbwana Makatta aliwashinda Mserbia Goran Kopunovic aliyekuwa Simba SC na Mholanzi Hans Van Der Pluijm wa Yanga SC katika tuzo ya kocha bora, baada ya kuinusuru Prisons kushuka daraja na kuzawadiwa Sh. Milioni 8.6.
    Israel Nkongo aliwashinda Jonesia Rukyaa na Samuel Mpenzu katika tuzo ya Mwamuzi Bora na kupata Sh. Milioni 8.6, wakati Mtibwa Sugar imezipiga kumbo Mgambo JKT na Simba SC katika tuzo ya timu yenye Nidhamu na kuzawadiwa Sh. Milioni 17.2.
    Ilikuwa ni Alhamisi usiku na mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia alikabidhi hundi ya Sh. Milioni 80.4 kwa kuwa mabingwa, Azam FC Sh. Milioni 40.2 kwa kuwa wa pili, Simba SC Milioni 28.7 kwa kuwa wa tatu na Mbeya City Milioni 22.9 kwa kuwa nne.
    Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom, Kevin Twisa aliwapongeza washindi wote na akasema wataendelea kudhamini ligi hiyo waliyoanza kuidhamini mwaka 2002.
    Lakini watu waliguna, walibeza kuanzia ndani ya ukumbi- kwamba Bodi ya Ligi Kuu imechemka mno katika tuzo hizo.
    Vyombo vya Habari na wadau mbalimbali wamebeza na wengi wameonyesha kukatishwa tamaa na hali jinsi ilivyo.
    Bodi ya Ligi imetutia fedheha kubwa. Kati ya walioitwa bora katika usiku huo- sehemu moja tu walipatia, ufungaji bora kwa Msuva.
    Na nina wasiwasi, kama mfungaji bora angekuwa hachaguliwi kwa idadi ya mabao yake, nayo pia ingechakachuliwa.
    Tunaona nchi nyingi- Mchezaji Bora wa Msimu ni yule ambaye amekuwa Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi mara nyingi- Bodi ya Ligi ituambie ni lini Msuva alikuwa Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi?
    Kama kumbukumbu zangu zipo sahihi, Joseph Mahundi wa Coastal ndiye mchezaji pekee aliyerudia kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu msimu huu, Desemba 2014 na Mei 2015.
    Basi huyu ndiye Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ingawa hayumo hata Taifa Stars B.
    Kuhusu refa sina shaka na Nkongo, lakini hiyo pia Bodi imebahatisha tu au kunaweza kukawa na mipango mingine vile vile.
    Makatta amepewa ukocha bora kwa sababu alikwenda Prisons zikiwa zimebaki mechi tano na akafanikiwa kuiwezesha timu kubaki Ligi Kuu.
    Bado hiki hakitoshi kuwa kigezo cha kumpa ukocha bora kama ameiongoza timu kwa mechi tano tu kati ya 26 za msimu.
    Hatukumtendea haki yule babu Mholanzi, Hans van der Pluijm aliyeipokea Yanga SC kutoka Mbrazil, Marcio Maximo ikiwa inashika mkia hadi kutwaa ubingwa.
    Aliyeipokea Yanga kutoka kwa Maximo ikiwa inacheza soka ‘mbofu mbofu’ hadi kuwa timu tishio- Pluijm ndiye kocha Bora wa Msimu wa Ligi Kuu. Huyo wa Bodi ni wao.
    Shaaban Kado anawezaje kuwa kipa bora wa msimu mbele ya Aishi Salum Manula aliyedaka karibu msimu wote Azam FC na kuiwezesha timu kushika nafasi ya pili?
    Unamzungumzia kipa chipukizi, ambaye yupo katika timu ya taifa na kipa tegemeo wa timu za vijana na wengi wanamtabiria kuwa tegemeo la taifa baadaye, Aishi Manula.
    Watu wanajua Aishi ni kipa aliyekuwa na msimu mzuri Azam FC na kipa aliyedaka mechi nyingi zaidi kati ya makipa wa timu tatu zilizokuwa zinagombea ubingwa, Yanga, Azam na Simba.
    Aishi Manula ndiye kipa bora wa Msimu wa Ligi Kuu, huyo Shaaban Kado ambaye timu yake ilipigana dakika za mwishoni kuepuka kushuka daraja ni kipa bora wa Bodi.
    Hakika tuzo za mwaka huu zilikuwa zina mushkeli mzito- hadhi yake ilikuwa ya chini, maandalizi hayakuwa mazuri na mambo mengi yalikuwa ovyo ovyo tu.
    Kuna kirusi kimeingia Bodi ya Ligi, tena kirusi kibaya sana ambacho sasa kinawatukanisha Bodi nzima, TFF yote na soka ya Tanzania yote kwa ujumla.
    Ndiyo, unadhani yule babu Pluijm ambaye anaamini kabisa alistahili kuwa kocha bora na akavalia suti yake nyeusi nadhifu, akitarajia atapewa tuzo atasema nini kwa upuuzi kama huu?
    Tunajihurumia Watanzania, tunafanywa wajinga na wanasiasa wetu na sasa tunafanywa wajinga na Bodi ya Ligi pia? Hivi watu wanafikiri Watanzania ni wajinga kiasi gani? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HIVI WATU WANAFIKIRI WATANZANIA NI WAJINGA KIASI GANI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top