• HABARI MPYA

    Monday, June 29, 2015

    ENDELEA KUTUSUTA BANZA STONE

    HATA siku mbili hazikupita tangu Jumatatu iliyopita nilipoandika kuwa “Tusisubiri Banza Stone atutoke ndo tukumbuke thamani yake.” Mambo yakajibu.
    Mambo yakajibu kivipi? Yalijibu kwa sababu Jumanne usiku, mjinga mmoja aliibua uvumi wa kifo cha Banza Stone, wajinga wengi, wenye pupa wengi, wapenda sifa wengi na wavivu wengi  wakaupokea ujinga ule na kuusambaza kwa fujo.
    Tukajitahidi kuzikanusha habari hizo, wenye kuelewa wakaelewa, lakini vichwa vya panzi wengine wakaamka tena na uzushi huo na kuzisambaza kwa kasi ile ile.
    Tukaanza kuona mabango mengi ya R.I.P (pumzika kwa amani) kupitia mitandao ya kijamii huku yakisindikizwa na sifa kibao.
    “Tutakukumbuka Daima Banza Stone”, “Tangulia Mwalimu wa Mwalimu”, “Pengo lako halitazibika”, “Mwanamapinduzi wa muziki wa dansi”. Hayo ni baadhi ya maneno niliyokutana nayo kwenye mtandao wa facebook na baadhi ya blogs.
    Kila mtu akaijua thamani ya Banza Stone, kila mtu akakumbuka umuhimu wake, kila mmoja akajidai kushtuka …huu ulikuwa msuto wa kiaina kupitia jina la Banza Stone. 
    Naam ni msuto unaotuonyesha namna Watanzania wengi tulivyo wanafiki, mtu unapokea simu zaidi ya 20 kwa watu wanaotaka kujua kama kweli Banza Stone kafariki, lakini miongoni mwa watu hao, labda ni wawili au watatu tu waliowahi kukupigia kutaka kujua Banza yu hali gani …inakera sana.
    Siku chache kabla sijaandika makala yangu ya wiki iliyopita, Banza aliniambia yupo tayari kupokea msaada lakini sio msaada wa matangazo (unatoa kisha unaanza kujinadi nimemsaidia Banza). 
    Lakini pia Banza aliniuliza: “Hivi ni kwanini watu wanapenda kunizushia kifo kila siku?” Swali hilo kaniuliza Jumamosi, Jumanne yakajitokeza hayo hayo aliyoniuliza …Hatari sana.
    Hao ndio wabongo, wala hawachoki kusutwa, maana wangekuwa wanachoka kusutwa basi haya ya Banza yasingejirudia, hii ni zaidi ya mara 20 Banza Stone anazushiwa kifo, tabia hii haikuanza leo wala jana ilianza zamani sana tangu mwaka 2007 ambapo mwimbaji huyo nyota wa muziki wa dansi alianza kuzushiwa kifo enzi hizo akiwa na bendi ya Twanga Chipolopolo.
    Wakati mwimbaji Amigolas anafariki dunia mwezi Novemba mwaka jana, mimi nilikuwa wa kwanza kumfahamisha Banza Stone, ilikuwa pale Magomeni kwenye ukumbi wa Flamingo Bar ambapo nilimwambia Amigo amefariki dunia usiku huu, Banza akashtuka sana.
    Unajua alichosema? Banza aliniuliza: “Kafa kweli? Maana wabongo kwa kuzusha ni balaa, mimi mwenyewe wamashaniua mara 50”.
    Hiyo ndio dhahama anayokutana nayo Banza Stone …‘anauliwa’ mpaka anazoea ‘kufa’ kiasi kwamba hashtuki tena akisikia ujinga huo, ndio kwanza  ujinga huo unampatia picha namna msiba wake utakavyopokewa na Wabongo.
    Hebu tujirudi na kujiuliza ni wangapi waliokuwa wazima wa afya, lakini wakafariki na kuwaacha wagonjwa mahutiti wakiendelea kuvuta pumzi ya mola wetu, imetoka wapi hii dhana ya mgonjwa lazima afe.
    Hussein Jumbe aliwahi kuimba “Nani Kaiona Kesho” akaasa kuwa tujifunze kuwajali na kuwatembelea wagonjwa badala ya kusubiri wafariki ili tujitokeze na makamera ya video na mambo mengine mengi ya kifahari. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ENDELEA KUTUSUTA BANZA STONE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top