• HABARI MPYA

    Sunday, June 21, 2015

    MKWASA AIKUBALI TAIFA STARS ‘KIMEO’, LAKINI ASEMA…

    Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
    KOCHA Msaidizi wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba anasubiri barua rasmi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya uteuzi wa kuwa kaimu kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars.
    Kiungo huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba amekwishasikia 'fununu' hizo na hana tatizo lolote, lakini anasubiri barua rasmi.
    Mkwasa alisema kwamba anasubiri taarifa rasmi kutoka TFF na kama kocha wa mpira hawezi kukataa jukumu hilo la kuiongoza Stars.
    "Nimeshasikia na jukumu hilo naliweza, ila tusubiri mpaka TFF watakaponitangaza rasmi", alisema Mkwasa.
    Charles Boniface MKwasa 'Master' amesema kwamba anasubiri barua rasmi ya uteuzi wake kuwa kocha wa Taifa Stars

    Kamati ya Utendaji ya Shirikishi la Soka Tanzania (TFF) jana ilimfuta kazi kocha wa Taifa Stars, Mholanzi, Mart Nooij na habari zinasema Mkwasa atashika timu kwa muda, akisaidiwa na Suleiman Matola wa Simba SC. 
    Kamati ya Utendaji ya TFF ililazimika kufanya kikao cha dharula baada ya Stars kufungwa mabao 3-0 na Uganda usiku wa jana Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika mchezo wa kwanza Raundi ya kwanza kufuzu CHAN 2016. 
    TFF italazimika kumlipa Nooij dola za Kimarekani zisizopungua 125, 000 (Sh. Milioni 250,000) kwa kumvunjia Mkataba, ambao ni mishahara yake ya miezi 10, kwa sababu kwa mwezi alikuwa analipwa dola 12,500 (Sh. Milioni 25).
    Mabao mawili ya mshambuliaji Erisa Sekisambu na lingine la Farouk Miya yanahitimisha historia ya kocha huyo Mholanzi Tanzania. 
    Habari za ndani zinasema Mkwasa na kocha Msaidizi wa Simba SC, Suleiman Matola watapewa timu kwa muda- mtihani wao wa kwanza ukiwa ni kujaribu kushinda mabao 4-0 ugenini wiki mbili zijazo ili kusonga mbele CHAN. 
    Matokeo ya jana yamewakosesha wachezaji wa Taifa Stars donge nono la Sh. Milioni 1 kila mmoja ahadi iliyotolewa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi jana.
    Mchezo wa jana ulikuwa wa tano mfululizo, Taifa Stars inafungwa chini ya Nooij aliyerithi mikoba ya Mdenmark Kim Poulsen Aprili mwaka jana na kwa ujumla timu hiyo imecheza mechi tisa bila ya ushindi chini ya Mholanzi huyo. 
    Kwa ujumla, Nooij ameiongoza Stars katka mechi 18 tangu arithi mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen Aprili mwaka jana, kati ya hizo ameshinda tatu tu, sare sita na kufungwa tisa- akifunga mabao 17 na kufungwa 28.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKWASA AIKUBALI TAIFA STARS ‘KIMEO’, LAKINI ASEMA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top