• HABARI MPYA

  Jumanne, Juni 30, 2015

  ZUTAH NA NGOMA WAMWAGA WINO YANGA SC MIAKA MIWILI KILA MMOJA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WACHEZAJI wapya wa kigeni wa Yanga SC, beki Joseph Tetteh Zutah kutoka Ghana na mshambuliaji wa Zimbabwe, Donald Ngoma wamesaini Mkataba wa miaka miwili kila mmoja leo kuichezea klabu hiyo.
  Katibu wa Yanga SC, Dk Jonas Tiboroha amesema kwamba wawili hao waliowasili Dar es Salaam Jumamosi asubuhi wamesaini Mikataba hiyo leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam.
  “Kwa kweli tumefurahi kukamilisha zoezi hili leo. Ni hatua moja katika kuimarisha kikosi chetu kuelekea msimu ujao,”amesema Tiboroha.
  Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC, Isaac Chanji akimshuhudia Zutah akisaini Mkatabaa leo
  Chanji akimshuhudia Ngoma akisaini Mkataba leo 

  Zutah aliyezaliwa Agosti 22, mwaka 1994 anatokea klabu ya Medeama ya kwao, wakati Ngoma anatokea FC Platinum ya kwao.
  Yanga SC iliitoa Platinum katika hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu, lakini kocha Mholanzi Hans van der Pluijm akavutiwa mno na Ngoma, aliyecheza mechi moja tu ya Zimbabwe baada ya kukosa mechi ya Dar es Salaam kwa sababu alikuwa majeruhi.
  Na Pluijm ambaye amewahi kufundisha Ghana, ndiye aliyempendekeza Zutah ambaye uongozi wa Yanga SC haujawahi kumuona kabisa, lakini vyanzo vinasema huyo ni mchezaji mzuri anayeweza kucheza pia kama beki wa kati na kiungo.
  Akiwa na umri wa miaka 26, Ngoma ni mchezaji mwenye uwezo na uzoefu mkubwa, kwani amekwishaichezea Zimbabwe hadi kwenye Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN).
  Januari 2014, kocha Ian Gorowa alimuorodhesha Ngoma katika kikosi cha Zimbabwe ambacho kilimaliza katika nafasi ya nne CHAN baada ya kufungwa na Nigeria 1-0 katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu mwaka jana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ZUTAH NA NGOMA WAMWAGA WINO YANGA SC MIAKA MIWILI KILA MMOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top