• HABARI MPYA

  Jumamosi, Juni 27, 2015

  YANGA SC YASAJILI ‘ZENJI ONE’ MIAKA MIWILI, WAKALI WA GHANA, ZIMBABWE WAWASILI PIA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imemsajili kipa namba moja wa Zanzibar, Mudathir Khamis kutoka klabu ya KMKM, aliyeitwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wiki hii.
  Katibu wa Yanga SC, Dk Jonas Tiboroha amesema Mudathir amesaini Mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo bingwa Tanzania Bara.
  Mudathir anafanya idadi ya makipa Yanga SC kuwa wanne, baada ya Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benedicto Tinocco.
  Hata hivyo, Tinocco aliyesajiliwa mwezi uliopita kutoka Kagera Sugar anaweza kutolewa kwa mkopo kwenda kukusanya uzoefu.
  Kutoka kulia ni Joseph Tetteh Zutah, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC, Aaron Mwinura Nyanda na Donald Ngoma baada ya kuwasili JNIA asubuhi ya leo

  Kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm ambaye wakati Tinocco anasajiliwa alikuwa likizo Ghana anakoishi, hajaridhishwa na uwezo wa mlinda mlango huyo na amependekeza atolewe kwa mkopo akapate uzoefu. 
  Wakati huo huo, wachezaji wawili wa kigeni wamewasili leo Dar es Salaam kuja kusaini mikataba ya kujiunga na Yanga SC.
  Hao ni beki wa kulia, Joseph Tetteh Zutah anayeweza kucheza pia kama beki wa kati na kiungo wa ulinzi kutoka Ghana na mshambuliaji Donald Ngoma kutoka Zimbabwe.
  Wawili hao walikutana Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi, Kenya asubuhi ya leo kila mtu akitoka nchini kwake na kuungana katika ndege ya KQ kuja Dar es Salaam.
  Walipokewa na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC, Mussa Katabaro, Aaron Mwinura Nyanda, Meneja Hafidh Saleh na Katibu Mkuu, Dk Jonas Tiboroha asubuhi ya leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.  
  Tiboroha akasema kwamba wachezaji hao wamekwishafikia makubaliano na klabu juu ya kusaini mikataba, zoezi ambalo litakamilishwa muda si mrefu.
  Hadi sasa, tayari Yanga SC imekwishasajili wachezaji watano wapya, ambao ni makipa Tinocco, Mudathir, beki Mwinyi Hajji Mngwali kutoka KMKM, kiungo Deus Kaseke kutoka Mbeya City na mshambuliaji Malimi Busungu kutoka Mgambo JKT.
  Ni mchezaji mmoja tu kutoka kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita, Mrisho Khalfan Ngassa aliyeondoka ambaye amehamia Free State Stars ya Afrika Kusini. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YASAJILI ‘ZENJI ONE’ MIAKA MIWILI, WAKALI WA GHANA, ZIMBABWE WAWASILI PIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top