• HABARI MPYA

  Jumatatu, Juni 22, 2015

  TUSISUBIRI BANZA STONE ATUTOKE NDO TUKUMBUKE THAMANI YAKE

  JUMAMOSI iliyopita majira ya saa 11 jioni nilitinga nyumbani kwa kina Banza Stone maeneo ya Sinza jijini Dar es Salaam ili kumjulia hali, nadhan wengi wetu tunafahamu kuwa mwimbaji huyo mahiri wa muziki wa dansi anaumwa.
  Nilipokewa vizuri kutokana na ukaribu na uenyeji wa kutosha nilionao kwa familia ya Banza, nikapata wasaa mrefu wa kuongea nae mambo kadha wa kadha.
  Tofauti na ilivyoripotiwa hapo awali kuwa Banza yu hoi na ameanza kupoteza uwezo wa kuongea, nilimuona swahiba wangu huyo kama mtu ambaye afya yake imeimarika na ana nguvu za kutosha za kupiga stori mpaka uchoke mwenyewe.
  “Mi niko fiti, naongea utadhani nina mp3 tumboni,” hiyo ilikuwa moja ya stori nyingi za Banza zilizonivunja mbavu. “Hii habari kuwa nimepoteza kauli sijui imetokea wapi, mbona watu wanapenda sana kunizulia mambo ya kufa kufa?” alinihoji Banza.
  Ukweli ni kwamba hali ya Banza inatia moyo lakini ana tatizo moja kubwa – nalo ni kukataa kumeza dawa pamoja na kuwa mbishi wa kula chakula.
  Banza anahitaji sana msaada kwenye hili – msaada wa kutembelewa na marafiki wake wa karibu ambao watakuwa na nguvu na ushawishi wa kumfanya akubali kula sambamba na kumeza dawa.
  “Ebwana hizi dawa zimenichosha sana, yaani unameza dawa mpaka unanuka dawa, kila anayeingia utasikia mpe dawa, mwingine akiingia naye utasikia mpe dawa, mmh hapana  mi nimechemsha,” hiyo ni kauli ya Banza akikiri kukataa kumeza dawa.
  Je Banza hajui madhara ya kukataa kumeza dawa?, hajui madhara ya kukataa kula? Je amejikatia tamaa? Jibu ni moja – Banza anahitaji ushauri, anahitaji upendo zaidi, anahitaji huruma, anahitaji kubembelezwa. Binafsi nilijaribu kumhamasisha ili aendelee kumeza dawa na akaniahidi kuwa kesho (jana Jumapili) angeanza upya kumeza dawa.
   “Tunajitahidi kumnunulia dawa ambazo ni ghali na zinatugharimu sana, lakini Banza hataki dawa wala hataki kula,” hiyo ni kauli ya mama mzazi wa Banza Stone.
  Nikapata wasaa wa kupitia maelezo ya dawa zake, Banza anahitaji kumeza jumla ya vidonge 15 kwa siku, achilia mbali dawa za kunywa, ni wazi kuwa zoezi hilo ni gumu na linahitaji moyo. 
  Tarehe 25 mwezi huu, Banza atarejeshwa hospitali kuonana na daktari wake ambapo huenda yakatolewa maelezo mapya ya dawa hususan kwa kuzingatia namna msanii huyo alivyovuruga dozi.
  Ni vema kuanzia hapo wadau na watu wa karibu wa Banza wakawa nae bega kwa bega, kumtembelea mara kwa mara, kumsaidia kwa hali na mali, kubadishana nae mawazo na kumhamasisha kwa yale yote yatakayokuwa na manufaa katika kuimarisha afya yake.
  Banza anasema kwa sasa hajiskii kuumwa sehemu yoyote ya mwili zaidi ya kuishiwa nguvu na kukosa hamu ya kula.
  Hebu tusahau yote yaliyopita, tusahau ukaidi wa Banza katika matumizi yake pombe, sigara na vitu vingine kama hivyo ambavyo siku zote vimekuwa ni adui mkubwa wa afya yake.
  Banza ni moja ya watu walioweka muhuri kwenye ramani ya muziki hapa nchini, tumpe heshima yake (hata kama yeye haitambui), tusisubiri atutoke ndiyo tuikumbuke thamani yake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TUSISUBIRI BANZA STONE ATUTOKE NDO TUKUMBUKE THAMANI YAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top