• HABARI MPYA

  Jumatatu, Juni 22, 2015

  NGASSA AJIFUA NA YANGA LEO KARUME, MASHABIKI 'WAPAGAWA'

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI mpya wa Free State Stars ya Afrika Kusini, Mrisho Khalfan Ngassa leo amerejea kwa muda katika timu yake kipenzi, Yanga SC na kufanya nayo mazoezi.
  Ngassa amefanya mazoezi na Yanga SC asubuhi ya leo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam na baada ya mazoezi mashabiki walisukuma gari lake hadi nje yaa geti kwa furaha, wakiimba; “Tutarudisha fedha (za Free State) urudi Yanga,”.
  Alipoulizwa mwenyewe sababu za kufanya mazoezi na Yanga SC leo, Ngassa alisema; “Yanga ni timu yangu, sijaondoka kwa ubaya, naweza kurudi wakati wowote,”.
  Hata hivyo, Ngassa alisema kwamba ameamua kufanya mazoezi na Yanga SC kujiweka fiti wakati anasubiri kutumiwa tiketi ya kurejea Afrika Kusini.
  Mrisho Ngassa akiwa mbele ya kocha Hans van der Pluijm mazoezini na Yanga SC leo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam

  “Nilipewa ruhusa ya kuja kuchezea timu ya taifa, bahati mbaya siku mbili kabla ya mechi na Uganda, nikaambiwa siwezi kucheza. Kwa hivyo, wakati nasubiri kutumiwa tiketi, nimeona nije kufanya mazoezi na Yanga kujiweka fiti,”amesema.
  Ngassa alisaini FS Mei mwaka huu Mkataba wa miaka minne baada ya kumaliza Mkataba wake wa miaka miwili Yanga SC akiiacha na ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Alhamisi Ngassa aliondolewa katika timu ya timu ya taifa iliyokuwa inajiandaa kwa mchezo wa kwanza dhidi ya Uganda Raundi ya Kwanza michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, baada ya Shirikisho la Soka  Afrika (CAF) kusema haruhusiwi kucheza kwa kuwa amekwishasaini Mkataba na timu ya Afrika Kusini, japokuwa hajaanza kuitumikia.
  Ngassa kulia kabisa akikimbia na wachezaji wenzake walioipa Yanga SC ubingwa msimu uliopita
  Ngassa kushoto akisikiliza mawaidha ya makocha wao leo Karume
  Ngassa kushoto akipiga mpira mbele ya makocha Pluijm na Charles Boniface Mkwasa

  Baada ya mechi na Uganda, ambayo Tanzania ilichapwa mabao 3-0, Ngassa amerejea Dar es Salaam na wakati anasubiri kutumiwa tiketi ya kurejea kazini Bethlehem, ameamua kufanya mazoezi ya kujiweka fiti na Yanga SC. 

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NGASSA AJIFUA NA YANGA LEO KARUME, MASHABIKI 'WAPAGAWA' Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top