• HABARI MPYA

    Friday, June 26, 2015

    HUYU NDIYE CHARLES BONIFACE MKWASA; KOCHA WA KWANZA MZALENDO STARS BAADA YA MIAKA TISA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MAPEMA wiki hii, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi alimtaja rasmi, Nahodha wa zamani wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa kuwa kocha mpya wa timu hiyo, badala Mholanzi, Mart Nooij aliyeondolewa. 
    Nooij aliyekuwa analipwa dola za Kimarekani 12,500 (zaidi ya Sh. Milioni 25) kwa mwezi, alifukuzwa mwishoni mwa wiki baada ya Taifa Stars kufungwa mabao 3-0 na Uganda Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Malinzi alitangaza rasmi Mkwasa kuwa kocha mpya wa Taifa Stars akisaidiwa na kocha Hemed Morocco na baadaye kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, maarufu kwa jina la utani akataja benchi lake zima.
    Mkwasa alimtaja mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ kuwa Mshauri wake wa Ufundi, Morocco Kocha Msaidizi, Manyika Peter kocha wa makipa, Mtunza Vifaa ni Hussein Swedi ‘Gaga’, Meneja Juma Mgunda na Mratibu Msafiri Mgoyi, wakati Daktari atatajwa baadaye.
    Mkwasa ambaye ni Kocha Msaidizi wa Yanga na Morocco kocha wa Mafunzo watafanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu ambayo timu ya taifa itakuwa katika kampeni za kuwania kufuzu CHAN na AFCON.
    Malinzi amesema uteuzi wa makocha hao wazawa umezingatia vigezo vya makocha wa timu ya Taifa kuwa na leseni A ya ukocha kutoka CAF au zinazofanana kutoka mashiriksho mengine duniani wanaozifanyia kazi, jambo ambalo makocha hao wazawa wamekidhi.
    “Kocha Mkwasa atakuwa akipewa hudumu zote na maslahi, zikiwemo posho alizokuwa anapewa kocha aliyeondoka (Nooij), nawaomba wadau wa mpira wa miguu na Watanzania kwa ujumla tuwape sapoti makocha hao wazawa,” aliongeza Malinzi.
    Mkwasa anakuwa kocha wa kwanza mzalendo kufundisha Taifa Stars tangu mwaka 2006, Profesa Mshindo Msolla alimpomuachia timu hiyo Mbrazil, Marcio Maximo aliyefanya kazi hadi 2010 akampisha Mdenmark, Jan Borge Paulsen, aliyempisha Mdenish mwenzake Kim Poulsen miaka miwili baadaye, ambaye naye Aprili mwaka jana alimuachia Nooij.
    Mkwasa ni kiungo hodari wa zamani wa kimataifa nchini na mume wa mwandishi wa habari na mtangazaji wa zamani wa Redio na Televisheni nchini, Betty Chalamila Mkwasa aliyeng’ara RTD na baadaye Redio One na ITV, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Dodoma.  
    Charles alizaliwa Aprili 10 mwaka 1955 mjini Morogoro, ambako alipata elimu yake ya Msingi na sekondari.
    Aliibukia katika timu ya Mseto FC ya Morogoro mwaka 1973 kama beki wa kati na kiungo hodari ambayo aliiwezesha kuwa timu ya kwanza kutoka nje ya Dar es Salaam kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania mwaka 1975.
    1976 akahamia Tumbaku pia ya Morogoro aliyoichezea hadi mwaka 1979 alipotua Yanga SC, wakati huo ikiwa imepoteza makali yake kufuatia mgogoro mkubwa wa mwaka 1976 ulioigawa timu hiyo na kuzaliwa Pan Africans.
    Baada ya nyota wengi wa Yanga SC kukimbilia Nyota ya Morogoro na baadaye kwenda kuasisi Pan Africans, timu hiyo ya Jangwani ikaanza kujiumba upya kwa kusajili nyota wengine, Mkwasa akiwa miongoni mwao.
    Akiwa na chipukizi wenzake wa wakati huo kama Ahmad Amasha, Juma Mkambi ‘Jenerali’, Mkwasa waliiwezesha Yanga SC kurejesha makali na kutwaa tena ubingwa wa Tanzania mwaka 1981 tangu walipotwaa mara ya mwisho 1974.
    Alidumu Yanga SC hadi mwaka 1989 alipoamua kutungika daluga zake za kuwa kocha mchezaji wa timu ya Super Stars ya Dar es Salaam. Lakini tayari mwaka 1988 alikwishaanza kupata mafunzo ya ukocha.
    Baada ya kozi tatu za awali za ukocha Tanzania, mwaka 1991 Mkwasa alikwenda Brazil alipochukua Diploma na aliporejea akajiunga na Yanga SC kama Msaidizi wa Syllersaid Mziray (sasa marehemu).
    Mkwasa ambaye mwaka 2000 alikwenda kusomea tena ukocha Ujerumani na kupata Diploma nyingine, kwa sasa ana leseni A ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) aliyoipata mwaka jana na pia ni Mkufunzi Daraja la Kwanza wa CAF tangu 2014.
    Mbali na kufundisha Super Star na Yanga SC kuanzia 1989 hadi 1993, Mkwasa alifundisha pia iliyokuwa timu ya Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), maarufu kama Sigara kuanzia 1994 hadi 1996 alipokwenda Al Khaboura ya Oman alikodumu hadi 1999.
    Alirejea nchini 1999 na kuwa Kocha Mkuu wa  Tanzania Prisons ya Mbeya, ambayo mwaka 1999 aliipa ubingwa wa iliyokuwa Ligi ya Muungano.
    Kwa mafanikio, Yanga SC wakamchukua kama kocha Mkuu mwaka 2001, akimrithi Raoul Jean Pierre Shungu kutoka DRC.
    Aliifikisha Yanga SC hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika ikatolewa na Mamelodi Sundwons ya Afrika Kusini baada ya kufungwa 3-2 ugenini na kutoa sare ya 3-3 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    Mwaka 2002 akahamia Coastal Union, 2003 akarejea Prisons alikodumu hadi 2005 alipohamia Moro United, kabla ya 2006 kuhamia Miembeni ya Zanzibar aliyoipa ubingwa wa Zanzibar na ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mbele ya vigogo wa Bara, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga SC.
    Mwaka 2008 akawa Kocha wa African Lyon kwa msimu mmoja kabla ya kuhamia Ruvu Shooting alikodumu hadi 2013 alipokwenda Yanga SC kama Msaidizi wa Mholanzi, Hans van der Pluijm.
    Mwaka jana baada ya msimu, akaondoka na Pluijm kwenda Al Shoolai ya Saudi Arabia, ambako hawakudumu, baada ya takriban miezi mitatu wakaacha kazi kufuatia kukerwa na kuingiliwa na uongozi wa timu juu ya masuala ya usajili.
    Desemba mwaka jana yeye na Pluim wakarejea Yanga SC kumpokea, Mbrazl Maximo na mwishoni mwa msimu wakaipa timu ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na kuifikisha hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika walipotolewa na Etoile du Sahel baada ya sae ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 1-0 Tunisia.
    Kwa mara ya kwanza kufundisha timu ya taifa ilikuwa ni mwaka 1993 alipoteuliwa kufundisha timu ya vijana chini ya umri wa miaka U17, kabla ya kuteuliwa kikosi cha pili Tanzania Bara, kilichopewa jina Kakakuona mwaka 1992, ambacho kiliwapiku ‘kaka zao’ Victoria 92 kwa kufika Fainali ya Kombe la Challenge, wakati huo akiwa Msaidizi wa Sunday Burton Kayuni.
    Mwaka 2001 alikuwa Msaidizi wa Mziray chini ya Mshauri wa Ufundi, Mjerumani Burkhad Pape katika kikosi Taifa Stars kilichotwaa ubingwa wa Kombe la mataifa manne, Castle Cup.  
    Mwaka 2002, yeye na Mziray waliifiksiha timu ya Bara fainali ya Kombe la Challenge na mwaka 2007 akapewa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kama Kocha Mkuu, lakini haikufanya vizuri baada ya kuambulia nafasi ya nne.
    Mwaka 2008 akapewa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars kama Kocha Mkuu ambako huko alipata mafanikio makubwa, ikiwemo kuiwezesha kukata tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika  mwaka 2010, Fainali za Michezo ya Afrika 2011 na kuwa washindi wa tatu Kombe la COSAFA pia mwaka huo.
    Mkwasa ni mshindi wa mataji ndani na nje ya Uwanja, akiwa anacheza alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara 1975 na Mseto, 1981, 1983, 1985, 1987 na 1989 na Yanga SC, Ligi ya Muungano 1983 na 1987, wakati pia walikuwa washindi wa pili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka 1986.
    Huyo ni Mchezaji Bora chipukizi wa Tanzania mwaka 1975 na Mchezaji Bora wa Tanzania mwaka 1981.
    Akiwa kocha, Mkwasa ametwaa mataji ya Ligi Kuu ya Bara katika miaka ya 1991, 1992, 1993 na 2015 akiwa na Yanga SC, Ligi ya Muungano 1991 na ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1993 mjini Kampala, Uganda.
    Ametwaa pia Ngao ya Jamii mara mbili, mwaka 2001 na 2014 akiwa na Yanga SC- na amekuwa Kocha Bora Tanzania mwaka 1999 na 2005.
    Huyo Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kocha wa kwanza wa Taifa Stars mzalendo baada ya miaka tisa. Je, atarejesha furaha kwa Watanzania? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.

    WASIFU WA CHARLES BONIFACE MKWASA;
    KUZALIWA: 10 Aprili 1955 (Miaka 60)
    ALIPOZALIWA: Morogoro, Tanzania
    NAFASI: Beki/Kiungo
    TIMU: Tanzania (Kocha Mkuu)
    KLABU ALIZOCHEZEA:
    Mwaka                      Timu                                      
    1973–1975               Mseto FC
    1976–1978               Tumbaku                  
    1979–1989               Yanga SC
    ELIMU YA UKOCHA
    1988: Kozi ya Awali
    1989: Kozi ya Kati
    1989: Kozi ya Juu
    1991: Diploma (Brazil)
    2000: Diploma (Ujerumani)
    HADHI ZA KITAALUMA;
    Ana leseni A ya CAF (Tangu 2014)
    Ni Mkufunzi wa CAF (tangu 2014)
    TIMU ALIZOFUNDISHA
    1989–1991   Super Stars   (Kocha Mkuu)
    1991–1993   Yanga SC       (Msaidizi wa Syllersaid Mziray)
    1994–1996   Sigara            (Kocha Mkuu)
    1998-1999    Al Khaboura (Oman, Kocha Mkuu)
    1999-2000    Tanzania Prisons
    2001-2002    Yanga SC
    2002               Coastal Union
    2003               Tanzania Prisons
    2005               Moro United
    2006               Miembeni
    2008               African Lyon
    2008-2013     Ruvu Shooting
    2013-2014     Al Shoolai (Saudi Arabia)
    2014:              Yanga SC
    TIMU ZA TAIFA
    1992-1993: Tanzania Bara B ‘Kakakuona’ (Msaidizi wa Sunday Kayuni)
    1993-1994; Tanzania timu ya vijana U17 (Kocha Mkuu)
    2001-2003: Tanzania Bara (Msaidizi wa Syllersaid Mziray)
    2007-2008: Tanzania Bara (Kocha Mkuu)
    2008-2013; Timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’, (Kocha Mkuu)
    2015-          Tanzania 'Taifa Stars' (Kocha Mkuu)
    MATAJI TUZO:
    WAKATI ANACHEZA; Ubingwa wa Ligi Kuu Bara; 1975 (Mseto), 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, (Yanga SC).
    Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati; 1986 (Washindi wa Pili)
    TUZO BINAFSI;
    1975: Mchezaji Bora chipukizi Tanzania
    1981: Mchezaji Bora Tanzania
    AKIWA KOCHA; 
    Ligi Kuu Bara; Ubingwa 1991, 1992, 1993, 2015 (Yanga SC)
    Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati; Ubingwa 1993 (Kampala, Uganda)
    Ngao ya Jamii; Ushindi 2001 na 2014 (Yanga SC)
    Kocha Bora Tanzania; 1999 na 2005
    TIMU ZA TAIFA;
    Ubingwa Kombe la Castle; 2001  (Taifa Stars)
    Tiketi ya Fainali za AFCON; 2010 (Twiga Stars)
    Washindi wa tatu COSAFA; 2011 (Twiga Stars)
    Tiketi ya Michezo ya Afrika; 2011 (Twiga Stars)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HUYU NDIYE CHARLES BONIFACE MKWASA; KOCHA WA KWANZA MZALENDO STARS BAADA YA MIAKA TISA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top